Makala

Ni vigezo gani vinafaa kutumika kuamua mtu ni mrembo?

August 23rd, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

MTAANI, wanaume wengi hukiri kuwa kivutio kikuu huwa ni wasichana “warembo.”

Hata hivyo, kwa uchambuzi wa kina, hii dhana urembo imewakanganya wengi kiasi cha kufanya uamuzi ambao baadaye walijutia kupata warembo machoni, lakini wenye tabia iliyooza.

Na ndipo swali linachipuka: Urembo wa mwanamke ni nini? Ni sura au ni tabia? Ni utu alio nao au ni umbo na hata uwezo wake wa kunengua au wa kujishasha?

Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya mapenzi, Gertrude Mungai, urembo ni jina la kina na sio la kuchezewa.

“Urembo ni jina kubwa. Jina lililo na ushawishi. Silo jina la mwanamume tu eti ameona mwanamke akipita akiwa na minisketi anaruka tu kusema muone yule mrembo. Utumizi wa jina mrembo kwa msingi wa minisketi au uwezo wa kunengua viungo vya mwili ni sawa na kulitusi hilo jina urembo,” anasema Gertrude.

Anasema hili jina urembo ni jina ‘takatifu’.

Anasema kuwa jina mrembo linaweza likatumika ghafla katika maamuzi na hukumu za ghafla kulingana na kile kimejisajili katika bongo lako katika zile hisia za kuangaliana na mwanamke.

“Ni kawaida mtu akimtazama mwanamke na aone miguu aliyo nayo ni ya kupendeza na kukosha, sura inavutia na viungo vya mwili vimejikata jinsi mwanamume atakavyo. Mwanamume anaweza kusema huyo ni mrembo, lakini ni muhimu ajifahamishe zaidi ajue tabia zake na mtazamo wake wa kimaisha ndiposa aamue huyu ni mrembo au ni mtu ovyo,” anasema.

Anasema kuwa urembo huchambuliwa kwa msingi wa yale mema kwa jamii, ya utu kwa binadamu na ubunifu wa kujiendeleza na kulea watoto.

“Mwanamke wa kujituma ni mrembo, awe na sura asiwe na sura. Kujituma kimaisha ili kujiendeleza na kuendeleza jamii na familia ni muhimu. Mwanamke ambaye hushikilia maadili ya kifamilia, kiimani na huwa na ule msukumo wa kusaidia jamii ni mrembo kupindukia,” anasema.

Anaeleza kwamba sampuli hiyo ya wanawake ni ile mwanamume atafurahia siku zote.

“Ni mwanamke ambaye ukiongea naye unaridhika. Unajihisi umetosheleka katika uhusiano wenu kwa kuwa ni mwanamke wa maono, mwenye akili pevu na aliye na ubunifu wa kutoa suluhu kunapotokea changamoto,” anaweka wazi.

Anasema kuwa wengi wa warembo hawajipodowi kwa kuwa wametosheka na jinsi Mungu muumba wa wote, yote na vyote aliwaweka uhai wao.

“Warembo wengi hung’ang’ania asilimia 100 ya uso wao kubakia jinsi Mungu alivyouumba. Mafuta kidogo tu na kuunawisha uso tu ni tosha. Sio aliumbwa akiwa mweusi lakini amejipodoa akisaka weupe kwa kujichubuwa,” anasema.

Bi Mungai anasema kuwa wanawake warembo hawang’ang’anii kutambulika au kupata umaarufu.

“Huonekana tu wakipita, wakiketi au wakishughulika bila kumkebehu yeyote katika hali zao za kimaisha. Urembo sio wa kuonekana tu bali ni wa kusikika na kugusika kihisia. Urembo huvutia wengi wakashuhudie. Sio kulazimishwa kuonekana na kuangazika. Urembo ni kama roho na hiyo roho ikivuma kutoka kwa huyo mwanamke, itavutia wengi kuifuata,” anasema.

 

Wanamitindo kutoka Kaunti ya Murang’a. Picha/ Mwangi Muiruri

Anasema kuwa warembo hujua jinsi ya kutumia ndimi zao kwa njia ya maongezi na ambapo maneno ya vinywa vyao hujenga wala sio kubomoa.

Anasema maneno ya warembo huwa na busara huku ya warembo bandia yakiwa ni ya kufuja pesa, kubomoa familia za wengine na pia kusambaza chuki na kushiriki udaku.

Mrembo hata aachwe na mumewe katika uhai wa maisha, atajikimu kimaisha kupitia maadili yanayokubalika.

“Hatangoja urithi wa kimapenzi au usambazaji wa mapenzi kwa wengine kiholela ili kujaza pengo hilo. Warembo watajipanga na katika maisha yao uwaone wakiweka maadili ya kimsingi na wakilenga kuishi maisha ya heshima. Hawatageuka kuwa hali sawa na mizinga michafu ya yeyote yule kurina asali,” anasema.

Anasema kuwa wanawake warembo ni vigumu uelewe kuhusu maisha yao ya ndani kwa kuwa wanajua kujiwekea yale yao ya kindani bila ya kuyasemasema ili yafichuke.

“Huo ni usiri wa kujitunza. Hawatakuambia ya ndani kuhusu maisha yao na ya walio wa karibu nao. Na pia wanajibeba kimaisha kama walio na ya umuhimu kutekeleza wala sio tu kukaa chini mjadili ya udaku,” anasema.

Anasema kuwa orodha ya uchambuzi huu ni refu na muhimu ni kwamba “usijichanganye katika kukumbatia urembo kwa kuwa urembo si sura bali ni uchambuzi wa kina kumhusu huyo unayetaka kuorodhesha kama mrembo.”