Habari MsetoSiasa

Ni vilio tupu katika ndoa ya Uhuru na Joho

October 1st, 2019 2 min read

VALENTINE OBARA na MOHAMED AHMED

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho sasa anakabiliwa na mtihani mgumu katika uhusiano wake na Rais Uhuru Kenyatta.

Hii ni baada ya Wapwani kukaidi misimamo yake kuhusu jinsi ya kusuluhisha changamoto wanazosema zimesababishwa na utumizi wa reli ya SGR kusafirisha mizigo kutoka bandarini.

Jana, wakazi, wakuu wa kampuni za uchukuzi wa mizigo, wanasiasa, mashirika ya kutetea haki za kibinadamu na wadau wengine walipuuza wito wa Bw Joho kwamba wanafaa kukumbatia mashauriano kusuluhisha changamoto zilizopo, wakaendeleza maandamano dhidi ya SGR, ambayo yamekuwa yakifanywa kwa wiki kadhaa sasa.

Wiki iliyopita, gavana huyo alikuwa amewaambia wakazi kwamba kutokana na urafiki wake siku hizi na Rais Kenyatta, milango i wazi kwake kufanya mashauriano na serikali kuu ili kilio cha Wapwani kisikilizwe na kusuluhishwa kikamilifu.

Lakini waandamanaji wamesisitiza, serikali lazima ijitokeze wazi kusema, wafanyabiashara hawatalazimishwa kutumia SGR kusafirisha mizigo yao kutoka bandarini bali watakuwa huru kutumia malori wanapotaka.

Bila hilo, viongozi waliokuwepo kwenye maandamano walitishia kushawishi wakazi wasusie sherehe za Mashujaa Dei ambazo zimepangiwa kufanyika Oktoba 20 zikiongozwa na Rais katika Bustani ya Mama Ngina iliyofanyiwa ukarabati.

“Sisi hatutabembelezana. Hatutakubali maziwa ya watoto wetu yapelekwe Naivasha. Leo tunafanya maandamano baada ya kila wiki moja. Wasiposikia tutaingia kila siku,” akasema Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali maarufu kama Jicho Pevu.

Wakati uchukuzi wa SGR ulipoanza kutekelezwa, Bw Joho alikuwa katika mstari wa mbele kuonya kwamba mtindo huo wa uchukuzi ungeweka hatarini uchumi wa Pwani.

Misimamo ya naibu kiongozi huyo wa Chama cha ODM ilimfanya kuwa hasimu mkubwa wa kisiasa wa Rais Kenyatta hadi akazuiliwa na polisi kuhudhuria uzinduzi wa SGR katika mwaka wa 2017.

Tangu Rais Kenyatta alipoingia mwafaka na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, imembidi Bw Joho kuboresha uhusiano wake na Rais, hali ambayo anasema imefanikisha miradi mingi ya maendeleo katika eneo hilo ndiposa anaamini pia kiazi moto cha SGR pia kinaweza kupozwa kwa mashauriano.

Gavana huyo mnamo wikendi alisema kuna mpango wa viongozi wa eneo hilo kukutana na Rais Kenyatta kwa mara ya pili mwezi huu kujadiliana kuhusu njia za kurekebisha hali ya kiuchumi ya eneo hilo.

Bw Joho alisema mkutano huo unatarajiwa kufanyika wiki moja kabla ya sherehe za Mashujaa.

“Rais mwenyewe amesema atakuwa huku wiki moja kabla ya Sikukuu ya Mashujaa, akatuambia sisi kama viongozi wa Pwani tuunde kamati yetu ya wataalamu na yeye atatupa kikosi chake cha wataalamu ili tufanye mkutano ambao atauongoza mwenyewe, na tuweze kupata suluhisho kwa matatizo yetu,” akasema Bw Joho.

Aliongeza kuwa mkutano huo utalenga kutafuta njia mbadala za kufufua uchumi wa Pwani ambao umedidimia.

Mkutano huo utakuwa wa pili baada ya ule wa kwanza ambao ulifanyika mapema mwezi uliopita kati ya Rais Kenyatta na viongozi hao wa Pwani wakiongozwa na magavana wote sita.

Baada ya mkutano, Kaunti ya Kwale ilijuzwa kuwa itasimamia bandari ya Shimoni wakati itakapomalizika.

Aidha, mipango ya kuweka depo katika Kaunti ya Voi nayo ikaonekana kufufuliwa kwa nguvu huku Kaunti ya Mombasa ikionekana kufaidi baada ya serikali kupata mkopo wa ujenzi wa daraja la Likoni na mradi wa sehemu ya kibiashara ya Dongo Kundu.

Bw Joho alisema ni kupitia mazungumzo yao ya awali ndipo miradi hiyo ikapangwa haraka.

Baadhi ya amri zinazotia wakazi tumbojoto katika SGR ni ile inayohusu usafirishaji mizigo kwa mtindo huo pekee, kwani wadau wakiwemo madereva wa malori na wamiliki wanahofia kumwaga unga.