Makala

Ni visiki vipi vinahujumu juhudi za kumaliza ukeketaji kabla ya 2030?

February 23rd, 2019 4 min read

Na MWANGI MUIRURI

KUNA viongozi wa kidini hapa nchini Kenya ambao huegemea mila na desturi za jadi katika jamii na ambao kisiri huunga mkono ukeketaji, hivyo basi kuhujumu vita dhidi ya ukeketaji wanawake, imeelezwa.

Pia, hali ni tofauti kabisa ambapo shughuli hiyo ambayo zamani iliendeshwa kisiri vichakani hasa huko mashinani, leo hii imekuwa ni biashara ya faida na ambapo kuna wauguzi ambao hulipwa ili kukeketa katika usiri wa vyumba vya kifahari na pia katika hospitali.

Haya yamefichuliwa na Shirika la Wanawake Waelimishaji Barani Afrika (Fawe), likisema kuwa waokovu hao hujumuika pamoja na wengine katika jamii walio na misimamo mikali inayoegemea uungaji mkono wa ukeketaji wa wanawake.

“Viongozi hao ambao wanajumuika katika dini kuu na pia zile za kibinafsi hapa nchini na huwa na uwiano wa kimaoni na makuhani wa dhati kuhusu ‘kukubalika’ kwa tohara hiyo, wote wakiishia kuwa na msimamo sawa na ule wa kundi haramu la Mungiki ambalo hupigia debe wanawake kukeketwa,” akasema Cecilia Njogu, mshirikishi wa Fawe nchini.

Bi Njogu anasema kuwa takwimu za 2018 zinaonyesha kuwa takriban wanawake 9.3 milioni nchini Kenya wanaishi na alama ya kukeketwa, hii ikiwa ni asilimia sita ya wote 140 milioni duniani ambao wanakadiriwa kuwa wako hai wakiwa na alama hizo.

Kuhusu wauguzi kuchangia utamaduni huu wa ukeketaji, bodi ya kupambana na ukeketaji wa wanawake nchini inasema kuwa ina ushahidi huo.

Aidha, kuna wakuu wa kiusalama ambao wamethibitisha kuwa wauguzi wengine wamejiunga na wale ambao wamekataa katakata kutupilia mbali tohara ya wanawake katika jamii lakini wao wakichochewa na tamaa ya kujipa pato.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Bi Agnes Pareyio anasema: “Hizi ni changamoto hatari na zilizo na ugumu sana kumenyana nazo, lakini uzuri ni kwamba serikali yote imejipa makataa ya hadi 2030 kuwe hakuna ukeketaji wa wanawakie nchini.”

Waziri aitisha ripoti

Anasema kuwa Waziri wa Usalama na Masuala ya Ndani, Dkt Fred Matiang’i tayari ameagiza bodi hiyo imkabidhi ripoti ya kuonyesha ni wapi utamaduni huo unashikiliwa kwa dhati na washukiwa wa njama hizo za ukeketaji.

“Ukiona Dkt Matiang’i ameingilia kati na ameanza kuwajibikia suala hili kwa karibu, basi tunapata imani kubwa kuwa tutapata mwamko mpya. Tuko na imani kuu kuwa kuna siku hivi karibuni ambapo ukeketaji utakuwa ukilaaniwa na wote katika jamii sawa na vile ugaidi hukemewa,” asema Bi Pareyio.

Katika siku ya kuadhimisha siku ya uhamasisho dhidi ya tohara ya wanawake ambayo iliadhimishwa Februari 6, mama wa Taifa, Margaret Kenyatta alisema kuwa serikali inachukulia suala hilo la ukeketaji wanawake kama changamoto kuu ya kiafya.

“Ni utamaduni ambao umepitwa na wakati na ambao katika sheria zetu, ni ujambazi. Nawahakikishia wadau wote kuwa serikali itabakia imejituma kuwamulika kwa ukali wote wa kisheria wote walio ndani ya sakata hii na ihakikishe wameshtakiwa na kufungwa vifungo gerezani,” akasema.

Naye Rachel Ruto ambaye ni mke wa Naibu Rais William Ruto,  alikemea tohara ya wanawake akiitaja kama ukatili mkuu dhidi ya mtoto msichana na kwa ujumla,  hujuma kwa wanawake duniani.

Bi Ruto aliwakumbusha wote walio ndani ya vitengo vya usalama kuwa Ibara ya 14 katika sheria ya kukinga watoto nchini Kenya kama ilivyotungwa 2001 hupinga moja kwa moja ukeketaji.

“Ukeketaji umeorodheshwa pamoja na maovu mengine kama ndoa za mapema, dhuluma za kimapenzi na pia mikakati yote ambayo nia ni kuhujumu uthabiti wa mtoto nchini. Wote ambao watapatikana wakihujumu sheria hiyo wamependekezewa adhabu ya kifungo cha juu kikiwa ni cha maisha gerezani,” akasema Rachel Ruto.

Bi Pareyio anasema kuwa sheria iko thabiti na kwamba kile ambacho kinafaa kuzingatiwa zaidi ni kujituma kwa maafisa wa usalama, viongozi wa tabaka mbalimbali katika jamii na pia familia zote nchini, kuwe na uwiano wa kukataa katakata ukeketaji wa wanawake nchini.

Tayari, Kamishna wa Embu, Bi Esther Maina ameonya kuwa ako na habari za ujasusi kuwa wanaoshikilia mila hiyo wanalipa wauguzi katika hospitali za Kaunti hiyo kuendeleza ukatili huo.

“Yule muuguzi ambaye anapania kujihusisha na ukeketaji wa wasichana aelewe kuwa jela inamngoja,” akasema Bi Maina.

“Usifikirie serikali ni jinga eti haijui vile njama ya ukeketaji inapangwa. Wewe ukiwa muuguzi hapa Embu, au popote kwingine nchini Kenya, jaribu kusajiliwa kwa pesa ushirikishe mila hiyo. Ukitaka kuhujumu taaluma yako na maisha yako ya kesho yako ukiwa jela, cheza na tohara ya wasichana hapa Embu,” akasema.

Aliwataka machifu na manaibu wao katika Kaunti hiyo wawe macho na wazime harakati zote za ukeketaji wa wasichana katika mipaka ya Embu.

“Nikisikia kuna msichana amekeketwa katika kijiji chako, wewe kama chifu na manaibu wako ndio nitakujia kwanza. Mzazi yeyote ambaye atashirikisha ukeketaji dhidi ya mnsichana wake pia nitakuwa na haja naye ili akamatwe na ashtakiwe. Hao wengine wote wa kushiriki dhuluma hiyo nitawanasa kwa uhakika,” akasema.

Bi Njogu anasema kuwa ikiwa dini zote hapa nchini hazitatoa msimamo wa hadharani kuwa “sisi ndani ya imani zote nchini kenya tunapinga kwa asilimia 100 ukeketaji,” basi hakuna uwezekano wa taifa hili kuafikia lengo lake la kutokomeza utamaduni huo kabla ya 2030.

Anasema kuwa shida kubwa ya hali hii ni kuwa, kanisa hutangamana na raia kwa siku nyingi kwa wiki mashinani na huwa na ile imani ya wengi katika jamii.

“Kanisa linaweza kuwa chombo muhimu cha kusaidia taifa kutokomeza tohara ya wanawake. Lakini hakuna kule kujituma ambao kumeshuhudiwa, na hii ni kwa sababu wengi wa viongozi wa makanisa haya huunga mkono ukeketaji kwa msingi wa kuendeleza utamaduni wa kijamii,” asema.

Kamishna wa Kaunti ya Narok ambapo mila hii hufuatwa kwa dhati anasema kuwa kuna familia nyingi sana hapa Kenya ambazo huishi katika makataa ya laana kuhusu ukeketaji.

“Kuna familia nyingi sana hapa Kenya ambazo kuna nyanya zao wa zamani ambao kabla ya kuaga dunia waliacha laana kuwa ni lazima jina lao katika vizazi liwe likitekelezewa tohara. Unapata kuwa familia leo hii ni ya kisasa, iko na waangwana ambao wamestaarabika lakini inawabidi kuwapasha tohara wasichana wote wao ambao wamepewa jina la yule nyanya aliyeaacha laana,” asema.

Anasema kuwa kuna wengine katika jamii ambao wanaamini kuwa wanawake ambao wamepashwa tohara huishia kuzimwa hisia za ngono kiholela na ambapo wataishia kuwa waadilifu katika jamii hasa katika ndoa zao.

“Hizo ndizo changamoto ambazo kwa sasa zinatukwamiza pakubwa katika mapambano dhidi ya kero hili. Serikali bado inasisitiza kuwa kukeketa msichana ni ujambazi sawa na wa kujaribu kuua na tukikupata  hatutazingatia kuwa uliachiwa laana au wewe huamini tohara hiyo husaidia nini katika jamii,” asema.

Anasema kuwa jami za Kimaasai katika kuviziana na serikali imebuni njama mpya ya kuvukisha wasichana hadi mataifa jirani na ambapo hutekelezewa tohara na hatimaye kurejea nchini wakiwa wameponesha majeraha yao.