HabariSiasa

Ni wakati wa 'Total Lockdown' Mombasa – Joho

April 24th, 2020 1 min read

Na CECIL ODONGO

GAVANA Hassan Joho wa Mombasa amependekeza kufungwa kabisa kwa Kaunti ya Mombasa kuzuia ueneaji zaidi wa virusi vya corona.

Hii ni baada ya kaunti hiyo jana kuripotiwa kuwa na visa 12 kati ya 17 vilivyothibitishwa na serikali jana.

“Jiji la Wuhan nchini China lilishinda janga la corona kwa sababu lilifungwa kabisa kuzuia maambukizi zaidi. Huu ni uamuzi mgumu tunaofaa kuchukua. Japo utatugharimu utatusaidia kuokoa maisha ya watu wetu,” akasema Bw Joho.

Waziri Msaidizi wa Afya Dkt Mercy Mwangangi alisema visa vingine vitano vilipatikana Nairobi.

Waziri pia alitangaza kupona kwa watu sita zaidi, na kufikisha idadi ya waliopata nafuu hadi 89.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe mapema wiki hii alisema virusi vya corona vimeenea katika kila mtaa wa Kaunti ya Mombasa, jinsi tu ilivyo Nairobi, ndiposa akawataka raia wazingatie usafi na kutilia manani maagizo ya Wizara ya Afya.

Kuhusu idadi ya jana, watu 15 waliopatikana na virusi hivyo hawakutoka katika vituo vya kuwatenga wanaoshukiwa kuwa navyo.

Wakati huo huo, Dkt Mwangangi alisema Wakenya waliotengwa hawafai kuchukulia suala hilo kama adhabu, mbali wanafaa kutii kwa sababu wao huruhusiwa kwenda nyumbani baada ya siku 14.

“Dalili ya virusi hivi huanza kujidhihirisha baada ya siku sita au zaidi kwa watu wengine. Ni vyema walio karantini wawe wavumilivu kwani wataruhusiwa kwenda nyumbani wakilamiza muda wao. Hii ni bora badala ya kutoroka kisha kusakwa na maafisa wa usalama,” akasema

Hata hivyo, Dkt Mwangangi na Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dkt Patrick Amoth walihepa swali la wanahabari, waliotaka kujua jinsi ambavyo mmoja wa watu waliotengwa alihepa na kupatikana Kericho, ilhali kuna marufuku ya kutotoka au kuingia Kaunti ya Nairobi.

Kufikia jana watu zaidi ya milioni 2.6 walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo kote duniani na elfu 186 kati yao kufariki.

Amerika iliendelea kuongoza ulimwengu kwa idadi ya maambukizi ikiwa na visa zaidi ya elfu 850 huku watu elfu 47 wakiaga dunia.