Ni wale wale wa ahadi hewa 2022

Ni wale wale wa ahadi hewa 2022

Na WANDERI KAMAU

WANASIASA wakuu wanne waliotangaza nia ya kuwania urais mwaka ujao hawana kipya cha kuwafaa Wakenya, utathmini wa rekodi zao za kisiasa unaonyesha.

Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM Raila Odinga, Musalia Mudavadi (ANC) na Kalonzo Musyoka (Wiper) wamejitokeza kama wawaniaji wakuu kwa ahadi za kuboresha maisha ya Wakenya wa kawaida hasa kiuchumi wakichaguliwa 2022.

Lakini rekodi zao katika siasa zaonyesha kuwa wanajifanya kujali maslahi ya mwananchi kila msimu wa uchaguzi, na mara wanapochaguliwa wanazingatia maslahi yao ya kibinafsi na ya washirika wao na jamaa.

“Kwa vigogo hao, siasa ni kama biashara. Ni jukwaa ambalo wamekuwa wakilitumia kujitajirisha, kulinda na kuendeleza maslahi yao ya kibinafsi. Ahadi ambazo huwa wanatoa nyakati za uchaguzi kuhusu mikakati ya kumsadia mwananchi ni njama za kuwapumbaza wapiga kura,” asema mdadisi wa siasa, Javas Bigambo.

Vigogo hao wanne wamekuwa katika bunge na serikali mbalimbali kwa jumla ya miaka 128, ambapo wameshikilia vyeo vya juu vilivyowapa nafasi za kutekeleza ajenda za kumsaidia mwananchi, lakini hawakufanya hivyo.

Wote wamewahi kuwa makamu wa rais isipokuwa Bw Odinga, ambaye naye alishikilia cheo kikubwa zaidi cha waziri mkuu.

Wadadisi wanaonya kuwa Wakenya wasitarajie utawala tofauti na wa sasa iwapo watachagua mmoja wa wanne hao, kwani rekodi zinaonyesha maslahi ya mwananchi hayapo kwenye ajenda zao.

Kulingana Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa masuala ya kisiasa, mawimbi ya kikabila na kisiasa ndiyo yamekuwa yakiwafumba macho wananchi wengi kwa muda mrefu nyakati za uchaguzi.

Dkt Ruto ana ufuasi mkubwa wa kikabila miongoni mwa jamii za Rift Valley, Bw Odinga ana ngome yake Nyanza, Bw Mudavadi (Magharibi) na Bw Musyoka (Ukambani).

Katika chaguzi za awali, wapiga kura wamekuwa wakiwachagua kwa wingi wawaniaji urais kutoka makabila yao bila kuzingatia sera zao.

Mdadisi wa siasa Prof Macharia Munene naye anasema kuwa wananchi wana uwezo wa kumaliza mtindo huo kwa kuwachagua viongozi kwa kuangazia sifa za utendakazi wao.

“Kenya ilikuwa na nafasi sawa kiuchumi na mataifa kama Singapore na Malaysia katika miaka ya sitini. Hata hivyo, nchi hizo zimepiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na uongozi bora. Ingawa huenda ikawa vigumu kwa Kenya kwa sasa, huo ndio mwelekeo ambao wananchi wanapaswa kuzingatia kwenye uchaguzi ujao,” akasema Prof Macharia kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Kwame Owino, anasema kuwa baadhi ya ahadi za vigogo hao kuhusu watakavyofufua uchumi wa nchi huenda isitimie.

Anasema kuwa wengi wao hawaelezi jinsi wayakavyopata fedha za kutimiza ahadi wanazowapa Wakenya.

Bw Owino anasisitiza kuwa kabla ya kuweka wazi watakavyotatua matatizo hayo mawili, vigogo hao wanawadanganya Wakenya, akieleza kuwa fedha za kuendesha uchumi haziwezi kupatikana kupitia ushuru pekee.

Kwenye uzinduzi wa manifesto ya Muungano wa Jubilee mnamo 2013, Dkt Ruto aliwaahidi Wakenya kuwa ikiwa wangeichagua Jubilee, huo ndio ungekuwa mwanzo wa “mapambazuko mapya” katika maisha yao.

Miaka tisa baadaye, maisha yamekuwa magumu zaidi huku wengi wakishindwa kutimiza mahitaji ya kimsingi kama vile chakula, kuelimisha watoto na afya.

Kwa upande wake, Bw Odinga bado anasisitiza kuwa ndiye mwenye ufunguo wa kutatua matatizo yanayowakumba Wakenya, licha yake kushindwa kufungua milango ya maisha bora kwa mwananchi tangu 1992 alipochaguliwa Mbunge wa Langata.

Bw Mudavadi naye amekuwa mkosoaji mkubwa wa sera za uchumi za serikali ya Jubilee, na anajiuza kwa Wakenya kama aliye na suluhu kwa matatizo wanayopitia Wakenya kwa sasa hasa madeni na gharama ya juu ya maisha.

Bw Musyoka alijitosa katika siasa mnamo 1985 na amehudumu akiwa mbunge, waziri na makamu wa rais, lakini licha ya kuahidi kuwa na ‘dawa’ ya matatizo ya Wakenya, rekodi yake haina cha kumtilia matumaini.

You can share this post!

Fiji wahifadhi nishani ya dhahabu kwenye raga ya Olimpiki

Covid-19: UN yarai mataifa kuanza kufungua shule zao