Makala

Ni wazi sasa ahadi za Jubilee kwa vijana zilikuwa hewa

August 20th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

Mei 2020 Rais Uhuru Kenyatta alipotangaza kuzindua mradi wa Kazi Mtaani ili kusaidia vijana wasio na kazi na ambao wameathirika kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona nchini, mamia na maelfu walijitokeza kujaribu bahati yao.

Mpango huo na ambao mwezi Julai uliingia awamu ya pili, unasemekana kulenga kunufaisha zaidi ya vijana 270, 000 wasio na ajira, walio kati ya umri wa miaka 18 – 35.

Suala la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana nchini linaendelea kuwa kikwazo na donda ndugu, mamia na maelfu wakifuzu kila mwaka kwa vyeti vya taaluma mbalimbali kutoka taasisi za juu za masomo.

Ukosefu wa kazi kati yao, umechangia wengi kushiriki visa vya uhalifu, unywaji wa pombe na matumizi ya mihadarati na dawa za kulevya, mitandao ya matukio inayowahatarishia maisha.

Ukizuru mitaa mbalimbali nchini, taswira ni ileile moja, hususan kwenye vibanda vya kutafuna miraa na pia kwenye vilabu. “Hiyo ni ishara ya kutelekezwa na serikali, kwa sababu hawana ajira. Ni picha inayopaswa kutia viongozi wasiwasi,” anaeleza Antony Kibui, 35.

Licha ya serikali ya Jubilee kudai inajikakamua kupiga jeki vijana, kulingana na Antony ambaye ni mfanyabiashara Nairobi, sauti ya vijana imepuuzwa.

Akitumia mfano wa uteuzi wa nyadhifa mbalimbali serikalini, haoni jinsi vijana wamewakilishwa. “Rais anapofanya uteuzi, hushangaa kuona ni wazee pekee wanaorejeshwa serikalini. Tutasikika lini? Suala la ukosefu wa kazi miongoni mwetu litatatuliwa lini ikiwa waliostaafu ndio wanaajiriwa tena na kuteuliwa?” Antony anashangaa.

Mashirika na kampuni mbalimbali, yakiwemo ya kiserikali yanapotangaza nafasi za kazi mahitaji ya tajiriba ya kutosha na ya muda mrefu ni kizingiti kikuu kwa vijana, Antony akihimiza bunge kupitisha sheria zitakazowasaidia kutofungiwa nje.

Kwa sababu ya ukosefu wa ajira, wengi wana ari ya kuwekeza kwenye biashara ila mtaji hawana. “Wakati wa usomaji bajeti kila mwaka, vijana hawakumbukwi katika mgao wa fedha. Pesa zinazosemekana ni za vijana hazitufikii,” analalamika Edward Kamangara, ambaye ni mchoraji hodari.

Mwanasanaa Edward Kamangara, ni mchoraji hodari. Anasema vijana waliojaaliwa vipaji mbalimbali wametelekezwa na serikali. Picha/ SAMMY WAWERU.

Serikali imekuwa ikihamasisha vijana kuchukua mikopo ya serikali, lakini kulingana na kijana Kamangara, taratibu na mikakati iliyowekwa inawafungia nje.

“Ukiniitisha dhamana ya hatimiliki ya shamba au cheti cha kumiliki gari ili unipe mkopo, nitatoa wapi? Hicho ni kichocheo cha ufisadi, unaoendelea kufuja fedha za umma na zinazoweza kutatua suala la ukosefu wa kazi kati yetu,” Kamangara anaiambia ‘Taifa Leo’.

Wengi wamejaaliwa vipaji tofauti, wanavyoweza kuvitumia kujiimarisha kimaisha na kimaendeleo, ila mtaji wa kuvipalilia hawana. Isitoshe, asasi husika zinaendelea kupuuza vijana wenye talanta, badala ya kufanya hamasisho kuwainua.

Ni mashirika machache mno nchini yaliyojitwika jukumu la kuangazia masaibu yanayokumba vijana.

Wakati wa kampeni, kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017, kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi aliibua mjadala: “Ni jambo la kuatua moyo kati ya Jumatatu hadi Ijumaa viongozi wa kisiasa kuandaa mikutano ya hadhara wakitafuta kura, kisha ukumbi, nyanja au bustani kama Uhuru Park zinajaa vijana.”

Bw Mudavadi alisema hiyo ni ishara kuwa vijana nchini hawana kazi, na ni ujumbe kwa serikali kufanya hima kuangazia suala hilo kabla maji kuzidi unga.

Mada ya mwaka huu wa 2020 katika maadhimisho ya siku ya kimataifa kwa vijana ni “Kuhusisha Vijana katika Maendeleo Ulimwenguni”. Mada hii ikiwa wazi “kushirikisha vijana kwenye maendeleo”, hapa nchini Kenya vijana wanaendelea kupuuzwa.

Mpango wa muda wa Kazi Mtaani, unaotajwa kusaidia kupiga jeki vijana kimapato, hata hivyo, unakosolewa na baadhi ya watu wakisema serikali inapaswa kuwapa ajira ya kudumu.

Aidha, wakosoaji wanahisi vijana wanahitaji suluhu ya kudumu ili kutatua kikwazo cha ukosefu wa ajira miongoni mwao, badala ya suluhu ya muda mfupi tu, kisha warejelee maisha magumu ya hapo awali.

Mradi wa Kazi Mtaani unahusisha usafi wa mazingira, hasa ufyekaji wa nyasi kandokando mwa barabara na njia, kuzoa taka, kuzibua mitaro ya majitaka, kati ya majukumu mengine ya kusafisha mitaa.

Waliopata fursa hiyo, wanalipwa mshahara wa Sh455 kila siku.