Maoni

Ni wazi wanasiasa wameanza kurejea katika jamii zao kujaribu kujiokoa kisiasa


WANASIASA wameanza kurejea katika jamii zao kujaribu kuokoa maisha yao ya kisiasa. Hii ndiyo sababu ya malumbano ambayo tunashuhudia kwa wakati huu hasa katika chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA).

Naibu Rais Rigathi Gachagua amekita kambi katika Mlima Kenya akiwaambia wakazi kuwa utawala aliosaidia kuunda umewapuuza.

Kinaya ni kwamba anafanya hivyo kwa kutumia rasilimali za serikali ambazo amepata kutokana na ushuru unaolipwa na wakazi anaodai kupigania maslahi yao.

Aliyekuwa mwenyekiti wa UDA, Johnson Muthama, naye amerudi kwa jamii yake akidai analenga kuiunganisha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Bila kugugumiza, mwanasiasa huyo alidai kwamba serikali aliyosaidia kuingia mamlakani imepuuza jamii ya Wakamba kuhusu nafasi za ajira serikalini kiasi cha yeye kupatiwa kazi ya utarishi.

Muthama ni kamishna wa Tume ya Huduma ya Bunge na anaonekana kuchukua msimamo sawa na Gachagua.

Inatarajiwa viongozi wengi watarudi kwa jamii zao wakijifanya kuzitetea uchaguzi mkuu wa 2027 ukikaribia.

Watatumia masuala yanayoathiri jamii kama sababu ya hatua yao hasa wakati huu ambapo gharama ya maisha imeathiri wananchi wengi.

Waliochangia hali hii wataanza mapema kama anavyofanya Bw Gachagua aliyekuwa mstari wa mbele kutetea utawala wa sasa.

Ukweli wa mambo ni kuwa wanasiasa waliochaguliwa wamegundua kuwa huenda nyota zao zikazima kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 na ndiyo sababu wanarudi mashinani mapema kujipanga upya wakijifanya kujali maslahi ya jamii zao.

Hii ni kufuatia malalamishi ya raia kuwa viongozi wao wanatumikia serikali badala ya kuwakilisha maslahi yao.

Siasa ni maslahi ya mtu binafsi anayetumia jamii kujifaidi na hii ndiyo huchangia kudorora kwa miradi ya maendeleo. Wakenya wawe tayari kwa vitimbi kutoka kwa wanasiasa!