HabariSiasa

Nia ya Ruto kutaka vyama vya NASA vivunjwe ni gani?

December 17th, 2018 2 min read

GERALD BWISA na WYCLIFFE KIPSANG

NAIBU Rais William Ruto, ameshauri viongozi wa upinzani wavunje vyama vyao ili wawe na chama kimoja kikubwa cha upinzani katika hali inayozua maswali kuhusu nia yake hasa.

Alitoa mfano wa chama cha Jubilee ambacho kilikuwa muungano wa vyama tanzu vinavyozidi 12 lakini vikavunjwa na kisha kukawa na Chama cha Jubilee ambacho kilitumiwa na Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita.

Ingawa Bw Ruto hakutaja vyama vya upinzani ambavyo angetaka viungane kuwa chama kimoja, muungano wa NASA ambao ulitumiwa na Kiongozi wa ODM Raila Odinga kuwania urais mwaka uliopita ndio ulio na vyama vikubwa vya upinzani nchini kufikia sasa.

Mbali na ODM, muungano huo una chama cha Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka, Ford Kenya kikiongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula, na Amani National Congress (ANC) cha Musalia Mudavadi.

“Umoja wa kitaifa unaweza tu kukuzwa kupitia kwa vyama vilivyo na nguvu wala si vyama vidogo vya kisiasa,” akasema Bw Ruto, alipohutubia waumini wa Dayosisi ya Kanisa Katoliki ya Kitale, katika uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Kitale jana.

Katika ziara yake, Bw Ruto alivumisha muafaka wa Rais Kenyatta na Bw Odinga, akisema ilikuwa hatua itakayoleta umoja katika taifa hili akatoa wito kwa Wakenya kuunga mkono umoja wa viongozi wa kisiasa.

Alitaka viongozi wote waweke kando siasa za kikabila na chuki ili kuendeleza nchi mbele.

Tushindane kuhusu sera, wala si siasa za chuki wala ukabila. Siasa tunayofahamu ni ile ambayo italeta umoja kwa Wakenya na kukuza maendeleo ambayo yatabadili maisha ya wananchi,” akaeleza.

Kuhusu suala tata la kilimo cha mahindi, Naibu Rais alisisitiza msimamo wake kuwa ni muhimu wakulima wa mahindi wawazie kuhusu ukuzaji wa mimea tofauti ili waepuke hasara ambazo zimezidi kushuhudiwa katika sekta hiyo.

Baadhi ya wabunge wamekuwa wakimkashifu kwa msimamo wake huo, wakisema anapotosha wakulima kwa maslahi ya mabwanyenye wachache ambao watapata mwanya wa kuingiza mahindi nchini kutoka mataifa ya kigeni kwa bei rahisi na kuyauzia serikali kwa bei ya juu kupita kiasi.

Lakini Bw Ruto alisema njia pekee ambayo itaepusha wakulima kulalamika baada ya kila msimu wa kuvuna mahindi, ni ikiwa watapanda mimea tofauti ya kilimo.

“Lazima tubadili njia zetu. Hatutakuwa tunapigania bei za mahindi kila mwaka. Ninataka kuwaambia muwakatae wale viongozi wanaopinga upandaji wa mimea tofauti kwani mtu kama huyo hafai hata kupewa nafasi ya kuchunga mifugo,” akasema.

Alieleza kwamba serikali tayari ina makubaliano na Uchina kupata soko la chai, makadamia, parachichi (avocado) na kahawa kwa hivyo wakulima wanafaa waanze kuzalisha mazao hayo ili wanufaike.