HabariSiasa

Nia yetu si kumng'oa Uhuru madarakani – Tangatanga

July 31st, 2019 2 min read

Na GRACE GITAU

WABUNGE wa chama cha Jubilee wanaomuunga mkono Naibu Dkt Rais William Ruto wamepuuza madai kwamba wanapanga njama ya kumng’oa Rais Uhuru Kenyatta madarakani kutokana na vita dhidi ya ufisadi vinavyoendelea kushika kasi nchini.

Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua na mwenzake wa Tetu Gichuhi Mwangi Jumanne walikemea matamshi yaliyotolewa na mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu kuwa wanapanga kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Rais Kenyatta bungeni, wawili hao wakisema ni kauli ya kipumbavu.

Mnamo Jumapili, Bw Wambugu alifichua kwamba baadhi ya wabunge wanaopinga vita dhidi ya ufisadi wamekuwa wakikusanya saini kabla ya kuwasilisha bungeni hoja hiyo ya kung’atua Rais.

Bw Wambugu pia alikashifu madai kwamba Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji na Mkuu wa Uchunguzi wa Makosa ya Uhalifu (DCI) George Kinoti walikuwa wakilenga jamii fulani kwenye vita dhidi ya viongozi wafisadi.

“Rais Uhuru Kenyatta anaendelea kutibua mtandao wa wafisadi ambao umekuwa nchini kwa miaka mingi ilhali wana ujasiri na fedha za kuandaa hoja ya kutokuwa na imani na utawala wake ili kumwondoa afisini. Vita dhidi ya ufisadi havilengi jamii fulani ila watu binafsi waliopora mali ya umma,” akasema Bw Ngunjiri.

Aidha aliyataja matamshi ya mbunge wa Kapseret Oscar Sudi ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto kwamba Rais ajiuzulu na amkabidhi mamlaka kwa muda wa miezi mitatu, kama ushahidi tosha kuwa kuna mipango ya kusambaratisha utawala wa sasa.

Hata hivyo, Bw Gachagua jana alisema wanamuunga mkono Rais kikamilifu na hawana mpango wowote wa kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani naye bungeni.

“Matamshi ya Bw Sudi hayafahi kuchukuliwa kwa uzito wowote kwa kuwa hayana mashiko. Watu kama Bw Ngunjiri wanaibuka tu na madai ili ijulikane wapo. Kila mara wanasema wanamtetea Rais, wanamtetea dhidi ya nani?,” akauliza Bw Gachagua.

Bw Mwangi naye alisema hajaona mbunge yeyote akikusanya saini bungeni wala hana habari iwapo kuna mpango wa kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na uongozi wa Rais Kenyatta bungeni.

“Hayo madai hayana msingi. Hakuna mbunge wa Jubilee amepanga kumbandua kiongozi wa chama madarakani,” akasema Bw Mwangi.