Michezo

Niasse kuondoka Everton

June 26th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI Oumar Niasse wa Senegal amethibitisha kwamba ataondoka rasmi kambini mwa Everton baada ya kandarasi yake kutamatika rasmi mwishoni mwa Juni 2020.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 alisajiliwa kutoka Lokomotiv Moscow ya Urusi kwa kima cha Sh1.9 bilioni mnamo 2016 ila akawajibishwa na Everton mara 65  pekee na akafunga jumla ya mabao 12.

Niasse alijivunia nusu wa msimu wa 2017 kambini mwa Hull City ambapo alifunga mabao matano kabla ya kuyoyomea Cardiff City kwa mkopo mwingine wa mwaka mmoja mnamo 2019.

Mbali na Niasse, masogora wengine ambao watakatiza rasmi uhusiano wake na Everton mwishoni mwa msimu huu ni mabeki Cuco Martina, 30, na Luke Garbutt, 27.

Wakati uo huo, beki Leighton Baines, 35, amekubali kutia saini mkataba mpya wa kipindi cha mwaka mmoja zaidi sawa na kiungo matata mzawa wa Ufaransa, Djibril Sidibe ambaye atasalia uwanjani Goodison kwa mkopo mwingine kutoka AS Monaco.