MWALIMU WA WIKI: Nicholas Kilonzo, mwalimu mahiri

MWALIMU WA WIKI: Nicholas Kilonzo, mwalimu mahiri

Na CHRIS ADUNGO

KUFUNDISHA wanafunzi wa shule za msingi ni kazi ngumu na rahisi!

Ni rahisi iwapo mwalimu – katika ufundishaji wake – atatumia mbinu zitakazompa jukwaa la kushirikiana na wanafunzi kutalii mazingira mbalimbali ya jamii inayowazunguka, kukuza viwango vya ubunifu na kuamsha ari ya kuthamini utangamano.

Haya ni kwa mujibu wa Bw Nicholas Kilonzo ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Kinderworld Academy, mtaa wa South C, Nairobi.

Akijivunia tajriba ya miongo miwili ya ufundishaji, Bw Kilonzo anaamini kuwa tija na fahari kubwa kwa mwalimu yeyote ni kuona mwanafunzi aliyeingia shuleni bila kujua lolote akipiga hatua kubwa kielimu na kuanza kufahamu stadi za kusoma na kuandika chini ya uelekezi wake.

Mbali na majukumu ya kawaida ya kufundisha, Kilonzo anahisi kwamba ni wajibu wa mwalimu kutambua na kukuza vipaji vya wanafunzi wake na kuwa tayari kuwasaidia kila wanapopitia changamoto mbalimbali.

“Tambua bidii ya kila mwanafunzi ndani na nje ya mazingira ya darasani. Wahimize wajitahidi zaidi katika hicho wanachokipenda kufanya. Jaribu kutambua kipaji cha kila mmoja wao na uwaelekeze ipasavyo kwa upole.”

“Mwalimu mkali hufanya wanafunzi wamwogope badala ya kumheshimu. Unapomfanya mwanafunzi kuwa rafiki wako wa karibu, atakuwa mwepesi wa kukufichulia panda-shuka zote anazozipitia. Nawe utapata fursa ya kubuni mbinu mwafaka za kumshajiisha na kumwezesha kufaulu katika kiwango chake binafsi,” anasema Kilonzo.

Kilonzo alizaliwa 1983 katika kijiji cha Vindungeni, eneo la Msambweni, Kaunti ya Kwale. Ndiye mwanambee (chudere) katika familia ya watoto wawili wa Bi Maria Nzilani na Bw Yohana Kilonzo Muia aliyewahi kuwa mwalimu kabla ya kuwa mkulima hodari wa matunda ya maembe na machungwa baada ya kustaafu.

Bw Nicholas Kilonzo wa Kinderworld Academy, South C, Nairobi. PICHA | CHRIS ADUNGO

Kilonzo alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Msambweni alikosomea hadi darasa la sita kabla ya kuhamia katika Shule ya Msingi ya Kilili, Kaunti ya Makueni.

Alitambua kipaji chake cha kutunga na kughani mashairi akiwa mwanafunzi wa darasa la saba na akaongoza shule kushiriki katika mashindano mengi nyakati za tamasha za kitaifa za muziki na drama chini ya uelekezi wa marehemu mwalimu Morris Makiti.

Baada ya kufaulu vyema katika mtihani wa kitafia wa KCPE, Kilonzo alijiunga na Shule ya Upili ya Kilili ambako kipaji katika sanaa ya uanahabari kilikuzwa na kupaliliwa vilivyo na Mwalimu Mainga. Shule hii ilimwandaa katika mchezo wa riadha na ubabe wake katika mbio za mita 400 ukamfanya maarufu sana miongoni mwa walimu na wanafunzi wenzake ndani na nje ya Makueni.

Baada ya kusomea ualimu katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha St Mark’s Kigari, Kaunti ya Embu (2008-2010), Kilonzo alianza kufundisha katika Shule ya Msingi ya Compuera, Nairobi.

Alihudumu huko kwa miaka mitano kabla ya kuhamia Shule ya Msingi ya Harambee katika mtaa wa Buruburu, Nairobi mnamo 2015. Ilikuwa hadi 2017 ambapo alijiunga na Kinderworld na akaaminiwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili mwaka mmoja baadaye.

Anashikilia kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano wa kiko na digali miongoni mwa walimu, wazazi na wanafunzi ni nguzo na mhimili wa mafanikio wanayojivunia kila mwaka katika mitihani ya kitaifa.

Zaidi ya kuwa mtunzi shupavu wa mashairi, Kilonzo pia ni mwandishi wa riwaya na tamthilia. Ndiye mwandishi wa riwaya ‘Dunia Yao’ na shairi tendi maarufu ‘Mambo Gani Haya?’. Aidha, ameandika tamthilia ‘Kisa cha Mkasa’. Kwa sasa anaandaa kitabu cha hadithi ‘Juhudi za Ufanisi’ kwa wanafunzi wa gredi ya tano.

Kilonzo amewahi kutuzwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG) baada ya kuibuka mwelekezi bora wa wanafunzi wake katika ‘Shindano la Uandishi wa Insha’ katika gazeti hili la Taifa Leo.

Kwa mujibu wa Kilonzo, wengi wa wanafunzi wake wanaothamini na kuchangamkia usomaji wa Taifa Leo kupitia mradi wa Newspapers in Education (NiE) na kushiriki Shindano la Uandishi wa Insha katika gazeti hili, hudumisha umahiri wao katika lugha kwa kukwangura alama za juu zaidi katika KCPE Kiswahili.

Anaungama kuwa majaribio ya mitahini katika Taifa Leo kila Jumatatu na Jumanne ni daraja halisi la mafanikio ya wanafunzi wake.

You can share this post!

PSG wazamisha St-Etienne na kufungua pengo la alama 12...

AS Roma ya kocha Jose Mourinho yashinda mechi tatu...

T L