Michezo

Nicholas Kipkorir aliandikisha muda bora Uholanzi

September 21st, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Nicholas Kipkorir Kimeli aliandikisha muda bora kwenye mbio za mita 10,000 mwaka 2020 baada ya kushinda makala ya 49 ya Golden Spike mjini Leiden nchini Uholanzi mnamo Septemba 19.

Kimeli,22, alimtika mizunguko hiyo 25 kwa dakika 26:58.97 na kumweka katika nafasi ya 60 kwenye orodha ya wakimbiaji 65 waliokamilisha umbali huo chini ya dakika 27.

Kabla ya hapo, Benard Kibet ndiye alikuwa mmiliki wa muda bora mwaka huu katika mbio za mita 10,000 baada ya kutawala shindano la Fukagawa nchini Japan alipolikamilisha kwa dakika 27:14.84 akifuatwa unyounyo na Wakenya wenzake Bedan Karoki (27:15.97) na Jonathan Muia Ndiku (27:23.47).

Rekodi ya dunia inashikiliwa na Muethiopia Kenenisa Bekele aliyetimka umbali huo kwa dakika 26:17.53 mwaka 2005. Paul Tergat (26:27.85), mwendazake Samuel Wanjiru (26:41.75), Eliud Kipchoge (26:49.02) na Geoffrey Kamworor (26:52.65).

Mkurugenzi wa mbio za Golden Spike Norbert Groenewegen aliridhishwa sana na matokeo ya Kimeli. “Siamini. Kama waandalizi wa mbio za Leiden, tunafurahi kuwa sisi sasa tunashikilia nambari moja katika muda bora wa mwaka huu,” alisema Groenewegen.

Matokeo (sita-bora): Nicholas Kipkorir Kimeli (Kenya) dakika 26:58.97, Solomon Kiplimo Boit (Kenya) 27:41.10, Mike Foppen (Uholanzi) 27:59.10, Emil Millan de la Oliva (Uswidi) 28:23.21, Stan Nielsten (Uholanzi) 28:30.81, Robert Keter (Kenya) 28:47.44