Michezo

Nigeria wasadiki ubingwa wa AFCON mara hii ni wao

June 6th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

NAHODHA wa zamani wa Super Eagles ya Nigeria, Joseph Yobo anaamini miamba hao wa soka wana kila sababu ya kutawazwa mabingwa wa Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019 hasa ikizingatiwa uwezo wa chipukizi watakaoongoza kampeni za kikosi hicho nchini Misri.

Yobo, 38, aliwahi kuwaongoza Nigeria kutwaa ufalme wa soka ya Afrika akivalia utepe wa unahodha wa kikosi hicho mnamo 2013. Ndiye mchezaji wa kwanza kuwahi kuvalia jezi za Super Eagles zaidi ya mara 100 katika historia ya soka ya Nigeria.

Nigeria wanarejea katika kampeni za kuwania taji la AFCON mwaka huu baada ya kukosa fursa ya kunogesha kivumbi hicho mnamo 2015 na 2017.

John Obi Mikel, Ahmed Musa na Kenneth Omeruo ni kati ya masogora walioongoza Nigeria kutwaa ubingwa wa AFCON mnamo 2013. Watatu hao watategemewa pakubwa na kocha Gernot Rohr kwa mara nyingine katika fainali za mwaka huu zitakazoandaliwa nchini Misri kati ya Juni 21 na Julai 19.

Japo Rohr amekosolewa pakubwa kwa hatua yake ya kuteua chipukizi wengi kupeperusha bendera ya Nigeria nchini Misri, Yobo anahisi kwamba ‘damu changa’ ya Super Eagles itawaduwaza wengi.

“Kocha ameteua kikosi ambacho anaamini kina uwezo, nguvu na ari ya kurejesha Nigeria katika ramani ya soka ya Afrika. Kikubwa zaidi ambacho sisi mashabiki tunastahili kufanya ni kumuunga mkono,” akatanguliza Yobo.

“Nimewahi kuwa katika kikosi kilichopigiwa upatu wa kutamba zaidi kutokana na ukubwa wa majina wa baadhi ya nyota waliowakilisha Nigeria katika fainali za AFCON mnamo 2002, 2004 na 2006. Lakini tuliloweza ni kuambulia nafasi ya tatu katika kila mojawapo ya makala hayo,” akasema.

Licha ya marehemu Stephen Keshi aliyekuwa mkufunzi wa Nigeria mnamo 2013 kukosolewa pakubwa kwa kuteua ‘kikosi kisicho na tajriba’ kuwakilisha Nigeria mnamo 2013, Super Eagles walishangaza wengi na kutawazwa mabingwa wa Afrika.

Kikosi cha Rohr kilichoanza mazoezi mnamo Juni 2 kinatarajiwa kukamilisha maandalizi yao mjini Asaba, Nigeria hapo Juni 9 kabla ya kuelekea mjini Ismailia, Misri kwa mchuano wa kupimana nguvu na Senegal hapo Juni 16.

Nigeria ambao ni mabingwa mara tatu wa taji la AFCON, wamepangwa katika Kundi B kwenye fainali za mwaka huu. Wapinzani watakaokutana nao jijini Alexandria wakati wa fainali hizo ni Guinea, Madagascar na Burundi ambao hii ni mara yao ya kwanza kushiriki fainali za AFCON. Nigeria watafungua kampeni zao za makundi dhidi ya Burundi hapo Juni 22 jijini Alexandria.

“Ilikuwa aibu sana kwa Nigeria ambayo ina zaidi ya raia milioni 200 kushindwa kufuzu kwa makala mawili yaliyopita ya fainali za AFCON. Kwa sasa tuna fursa ya kujinyanyua na kuwadhihirishia wakosoaji wetu uwezo tulionao,” akasema Yobo kwa kusisitiza kuwa chipukizi wa sasa wa Super Eagles watatua Misri bila presha yoyote.

 

Fowadi wa Nigeria, Ahmed Musa asherehekea baada ya kufunga bao lake la pili katika mechi ya fainali za Kombe la Dunia, hatua ya makundi, dhidi ya Iceland mwaka 2018 ugani Volgograd Arena mjini Volgograd, Urusi. Picha/ Maktaba

Yobo alishiriki mchuano wake wa 100 ndani ya jezi za timu ya taifa ya Nigeria mnamo 2001 dhidi ya Zambia jijini Chingola katika mchuano wa kufuzu kwa fainali za AFCON mnamo 2002.

Nyota huyo wa zamani wa Everton, Fenerbahce na Norwich City, amewahi kuchezea Nigeria katika fainali sita za AFCON kati ya 2002 na 2013 katika kipindi cha miaka 14 ya kupiga kwake soka ya kitaaluma.

Alikuwa pia sehemu muhimu ya kikosi cha Nigeria kilichoshiriki fainali za Kombe la Dunia mnamo 2002, 2010 na 2014.

Mbali na Mikel aliyekuwa nahodha wa Nigeria kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka jana, mchezaji mwingine anayetarajiwa kuwa nguzo kubwa katika kikosi hicho cha Super Eagles ni mvamizi matata wa Leicester City, Kelechi Iheanacho.

Iheanacho atakuwa na fursa ya kusaka bao lake la kwanza ndani ya jezi za Nigeria tangu Novemba 2017 alipofunga dhidi ya Argentina.

Mikel ambaye ni kiungo wa zamani wa Chelsea kwa sasa hana klabu baada ya mkataba wake na Middlesbrough kutamatika rasmi mwishoni mwa mwezi jana.

Rohr anatarajiwa kuchuja zaidi kikosi chake mwishoni mwa mechi ya kirafiki itakayowakutanisha na Zimbabwe apo Juni 8 na kusalia na wachezaji 23 pekee watakaoelekea Misri.