Habari MsetoSiasa

Niite nikufundishe jinsi ya kukabili madeni, Raila amwambia Rotich

September 8th, 2018 2 min read

Na MWANDISHI WETU

KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga sasa amemwitisha kikao cha dharura Waziri wa Fedha Bw Henry Rotich, amfundishe jinsi serikali inaweza kuimarisha mapato na kulipa madeni bila kuwapandishia Wakenya gharama ya maisha.

Bw Raila amemmtaka Bw Rotich amwite mezani wajadiliane kuhusu suluhu mwafaka za kukabiliana na deni la Sh5 trilioni ambalo limeisukuma serikali kuongeza ushuru kwa bidhaa za mafuta kwa asilimia 16.

“Tunajua kwamba tunaweza kupata suluhu tosha kwa masaibu yetu. Tulifanya hivyo wakati wa serikali ya muungano na aliyekuwa Rais Mwai Kibaki, tunajua jinsi tunaweza kupata suluhu. Nitampa Rotich ushauri bila malipo jinsi atasaidia nchi hii,” akasema kiongozi huyo.

Alielezea jinsi ongezeko la ushuru limefanya maisha kuwa mlima kwa wananchi wengi ambao sasa hawawezi kumudu bei ya petroli, dizeli na mafuta taa hali ambayo imechangia bidhaa za viwandani kupanda bei.

Alisema kuwa changamoto hizi hazifai kuzuia maendeleo ya taifa hili, kwa kuwa suluhu zinaweza kupatikana bila kuwasukumia wananchi gharama kubwa ya ushuru.

“Tunajua kwamba taifa letu linaumia kwa sasa. Ndiyo maana tunafaa kufanya mazungumzo kuhusu jinsi tutakavyomudu madeni yanayotukabili ambayo yanalazimisha serikali kuongeza ushuru,” akasema.

Akihutubu nyumbani kwake eneo la Opoda, Bondo, Kaunti ya Siaya, Bw Odinga alisema kwamba mazungumzo hayo yanafaa kuleta mbinu mbadala kwa serikali kuhusu kuongeza pato la nchi, bila kuwaadhibu Wakenya kwa makosa ambayo hawakufanya.

Alitoa wito kwa mashauriano kuanzishwa haraka ili suluhu ya dharura ipatikane na kupunguza gharama ya maisha ambayo sasa imeleta taswira ya uchumi ambao uko tayari kuporomoka.

Mwanasiasa huyo kigogo alisema kuwa ana imani kwamba viongozi wa nchi hii wana uwezo wa kusaka suluhu kwa mzigo wa kiuchumi unaolikodolea macho taifa.

Kulingana naye, serikali inafaa kuzidisha vita dhidi ya ufisadi, akieleza kuwa iwapo zimwi la ufisadi litazimwa, basi serikali inaweza kupata fedha bila kupandisha ushuru kwa wananchi.

“Maoni yangu ni kwamba lazima tumalize ufisadi kwanza. Pesa nyingi ambazo serikali hii hupata hupotelea kwa mifuko ya wafisadi. Tukikusanya ushuru wetu bila kuibwa na yeyote, tutaweza kujitegemea na uchumi kumfaa kila Mkenya,” akasema.

Licha ya Mahakama Kuu ya Bungoma kusitisha kwa muda utekelezwaji wa ushuru wa asilimia 16, bei ya mafuta vituoni haijashuka, na wanachokishuhudia wananchi ni kukauka kwa mafuta vituoni huku bei ya lita moja ya petroli ikigonga Sh150 kwa vituo vichache vyenye bidhaa hiyo.

Awali, Bunge la Kitaifa lilikuwa limedinda kupitisha mswada wa kuongezea ushuru kwa bidhaa za mafuta, likitaka hatua hiyo icheleweshwe kwa miaka miwili, lakini Wizara ya Fedha ikapuuza uamuzi wake na kupandisha ushuru.

Kwa sasa ili gharama ya maisha irudi kwa viwangi vya wastani, Kenya inahitaji Sh8 trilioni, Sh3 trilioni za kufadhili bajeti ya mwaka huu wa kifedha na zingine Sh5 trilioni za kulipa madeni ambayo inadaiwa na mataifa ya kigeni pamoja na mashirika ya fedha duniani.