Nike yafika mahakamani kushtaki kampuni kuhusu ‘viatu vya kishetani’

Nike yafika mahakamani kushtaki kampuni kuhusu ‘viatu vya kishetani’

Na MARY WANGARI

KAMPUNI ya kutengeneza viatu vya wanariadha, Nike Inc, mnamo Jumanne, Machi 30, 2021, ilishtaki kampuni moja ya New York, iliyounda ‘viatu vya kishetani.’

Viatu hivyo vinadaiwa kusheheni tone la damu kama sehemu ya ushirikiano na mwimbaji wa nyimbo za kufokafoka Lil Nas X.

Kupitia kesi iliyowasilishwa Jumatatu, Nike ilisema kuwa kampuni ya MSCHF Product Studio Inc, iliingilia na kudunisha nembo yake, kupitia viatu hivyo vyenye rangi nyeusi na nyekundu, vilivyo na maudhui ya kishetani.

Viatu hivyo viliuzwa mitandaoni siku hiyo ya kuwasilishwa kwa kesi ambayo haikumtaja Lil Nas X kama mshtakiwa.

“Viatu hivyo ni aina ya Nike Air Max 97 vilivyofanyiwa marekebisho na vinasheheni wino mwekundu na “tone moja la damu ya binadamu” kwenye wayo, kulingana na tovuti moja iliyofafanua viatu vya nambari ya kishetani ya 666.

Upande mmoja wa kiatu hicho umeandikwa “MSCHF” na huo mwingine umeandikwa “Lil Nas X.”

Viatu hivyo viliripotiwa kuuzwa vyote chini ya muda wa dakika moja kwa bei ya Sh111,471 kwa kila kiatu.

Lil Nas X, kupitia akaunti yake ya Twitter alisema atamchagua mnunuzi nambari 666 wa viatu hivyo miongoni mwa wanamitandao waliosambaza ujumbe wake kwenye Twitter.

Kupitia kesi iliyowasilishwa katika mahakama ya New York, Nike, ilisema viatu hivyo viliundwa bila “idhini na kibali cha Nike” na haihusiani kwa vyovyote na mradi huo.

“Tayari kuna ushahidi wa hali ya kuchanganyikiwa na kudunishwa kwa bidhaa sokoni ikiwemo wito wa kususia Nike kufuatia uzinduzi wa Viatu vya Shetani vya MSCHF kutokana na dhana potovu kuwa Nike imeidhinisha au kukubali bidhaa hii,” ilisema nakala ya kesi.

Nike imeiomba mahakama kuachisha MSCHF dhidi ya kuuza viatu hivyo na kuitisha kikao cha majaji ili kuomba fidia.

Rapa huyo mwenye umri wa miaka 21 ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Grammy, mnamo Ijumaa, Machi 26, 2021, alitoa video ya wimbo mpya kwa jina “Montero (Niiite Kwa Jina Lako)” ambamo anacheza densi na kiumbe kilicho na pembe za kishetani.

You can share this post!

Mbunge azishangaa hospitali za umma kusema hazina mitungi...

Hatimaye Ruto apokea chanjo ya corona