Habari Mseto

Nikilewa huwa ninatamani kila mwanamke

January 4th, 2024 1 min read

Kwako shangazi. Nina shida inayohitaji ushauri wako. Nikilewa pombe huwa mkarimu sana kwa wanawake. Kila tunayekutana nahisi kumpenda tu. Nikiingia baa na pesa nyingi hutoka bila chochote. Nishauri.

Jinsi moja ya kukabiliana na hali hiyo ni kuwa na mpenzi wa kuandamana naye kwenye ili kuepuka wanawake wengine. Jinsi nyingine ni kubeba pesa zinazotosha pombe yako tu unapoamua kuingia baa. Tafakari.

Huyu ananitafutia nini?

Mambo shangazi? Mpenzi wangu aliniambia alikuwa na mwingine lakini wakaachana. Sijui huyo mwingine alivyopata namba yangu ya simu. Ameanza kunitumia jumbe akiniambia niachane na mpenzi wake. Nishauri.

Kuna jinsi moja tu ya kutegua kitendawili kinachokukabili. Mwambie mpenzi wako amtafute huyo mwingine kisha mkutane ili mzungumze ana kwa ana. Ni kwa njia hiyo tu ambapo utamjua msema kweli.

Anapenda starehe sana

Salamu shangazi. Nimependana na mwanamke aliye na mtoto. Lakini mapenzi yake yananishinda. Anapenda maisha ya starehe na sina pesa. Sasa anatishia kuniacha. Nifanye nini?

Mapenzi ya dhati hayana masharti. Kwa kutishia kukuacha, mpenzi wako amethibitisha kuwa anahitaji mwanamume mwenye uwezo wa kugharamia mahitaji yake ya pesa. Kama huna uwezo huo achana naye.

Natamani asali lakini…

Salamu shangazi. Ni mwaka mmoja sasa tangu nipate mpenzi. Nimekuwa nikitaka burudani lakini naogopa kumwambia kwa sababu sitaki afikirie kuwa hiyo ndiyo nia yangu kwake. Nishauri.

Ni haki yako kumwelezea mpenzi wako mambo yote yaliyo moyoni mwako. Hilo ni jambo mnaloweza kushauriana na kuelewana. Inawezekana yeye pia anataka lakini ameshindwa kukwambia. Kama hajawa tayari atakwambia.