HabariSiasa

Niko tayari kufichua kuhusu mauaji ya Msando – Akombe

December 19th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Kamishna wa zamani wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) anayeishi Amerika Bi Roselyn Akombe amesema yuko tayari kuelezea maafisa wa ujasusi anayofahamu kuhusu mauaji ya kinyama ya aliyekuwa meneja wa Idara ya Teknolojia katika  IEBC mwendazake Bw Chris Msando.

Dkt Akombe anataka Afisi ya Mkurugenzi wa Ujasusi (DCI) kuanzisha uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo na kusema yuko tayari kutoa taarifa zote anazojua kuhusu kisa hicho.

Alisema hayo baada ya Mkurugenzi wa DCI Bw George Kinoti kuagiza kufanyika kwa uchunguzi kuhusu kifo cha aliyekuwa Gavana wa Nyeri Wahome Gakuru.

Katika akaunti yake ya Twitter, kamishna huyo wa zamani, na ambaye anafanya kazi na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) alisema, “Ninatazamia DCI kuanzisha uchunguzi unaohusisha umma kuhusiana na mauaji ya kinyama ya mwenzangu katika IEBC Chris Msando na Bi Ngumbu. Ninathibitisha nitakuwepo kuhojiwa chini ya kiapo.”

Bw Kinoti alikuwa ameshauri mahakama kuanzisha uchunguzi wa umma kuhusiana na kifo cha marehemu Gakuru, aliyeaga dunia katika ajali ya barabarani mwaka jana, miezi kadhaa baada ya kuapishwa kama gavana wa tatu wa Kaunti ya Nyeri.

Mwili wa marehemu Msando, ambaye alikuwa afisa wa habari, mawasiliano na teknolojia wa IEBC ulipatikana Jumatatu Julai 31, 2018 City Mortuary siku saba, kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Kulingana na rekodi katika mochari hiyo, mwili huo ulikuwa umewasilishwa humo Jumamosi, Julai 29, 2017 asubuhi.

Maafisa wa polisi walisema kuwa waliokota mwili huo pamoja na mwili wa Bi Caroline Ngumbu (uliokuwa umetupwa karibu kilomita moja mahali mwili wa marehemu Msando ulikopatikana) kichakani, eneo la Kikuyu.

Licha ya serikali kuahidi uchunguzi kuhusiana na kifo hicho, inakaa mauaji hayo yamesahaulika, zaidi ya mwaka mmoja tangu yalipotekelezwa.

Kwa upande wake, Dkt Akombe alijiuzulu IEBC siku chache kabla ya uchaguzi, na katika mahojiano baada ya kuondoka nchini kwa njia ya siri, alieleza kuwa alihofia usalama na maisha yake kwa sababu alikuwa akitishiwa.