Habari Mseto

Niko tayari kumuoa hata kama amezaa na mwanamume mwingine lakini bado ananikataa

May 6th, 2024 1 min read

Mambo Shangazi? Mpenzi wangu ana mtoto kutokana na uhusiano wa awali. Nimeamua kumuoa lakini ameniambia siwezi kumuoa akiwa naye. Anataka kumpeleka kwa babake. Waonaje?

Mtoto huyo si wako, kwa hivyo huwezi kumzuia mpenzi wako kupeleka kwa baba yake. Kama ameamua hivyo na inawezekana, mimi sioni tatizo lolote bora tu una uwezo wa kupata watoto wako.

Nimepata dude faya ila nahofia mzee akijua

Mume wangu hatoshi chumbani. Nimekuwa nikitoka nje kushughulikiwa na wanaume wengine. Licha ya udhaifu wake huo, ana wivu sana na akijua anaweza hata kuniua. Nifanyeje?

Maisha ya ndoa si ya lazima. Mbali na mume wako kugundua mienendo yako, unaweza kuambukizwa magonjwa. Ni heri umwambie ukweli ili mtafute suluhisho hata kama ni kuachana kisha utafute mwingine.

Rafiki hasidi ameniletea fitina mpenzi akaniacha

Mpenzi wangu aliniacha wiki mbili zilizopita baada ya rafiki yake kumwambia eti tuna uhusiano wa pembeni. Ukweli ni kwamba ni huyo rafiki amekuwa akinitaka lakini nimemkataa. Nifanyeje?

Ninaamini ulikataa kumwambia mpenzi wako kuhusu nia ya rafiki yake kwako ili wasikosane. Lakini sasa huna sababu ya kumhurumia. Mwambie ukweli liwe liwalo.

Sponsa wivu tu, anatisha kunikaushia hela

Shikamoo. Niligundua mpenzi wangu ni mume wa mtu na nikatafuta mwingine wa pembeni. Amejua na ameniambia nichague kati yake na huyo mwingine. Namtegemea sana kwa mahitaji yangu ya pesa. Nishauri.

Nahisi umekuwa mateka wa mwanamume huyo kwa sababu ya msaada wake. Ukiweka pesa mbele katika uhusiano wa kimapenzi utapotea. Tosheka na huyo mwingine na kidogo anachokupa.