Michezo

Nikome kuvuta sigara? Labda babangu anishawishi – Kocha wa Chelsea `

September 11th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Chelsea Maurizio Sarri amefichua kwamba ni babake (Amenga) pekee mwenye uwezo  wa kumshawishi kugura uraibu wa kuvuta sigara.

Sarri alitambuliwa sana nchini Italia akiwa kocha wa Napoli kutokana na uraibu wake wa  kuvuta sigara pembeni mwa uwanja wakati wa mechi za Serie A. Vile vile Sarri ametawaliwa na uraibu huo kiasi kwamba ni  mvutaji hodari ambaye hakosi kumaliza zaidi ya pakiti tano za dawa hiyo ya kulevya kila siku.

“Wakati babangu alipata taarifa kwamba nilipata ofa ya kujiunga na Chelsea, alinieleza nije mji wa London na kusema ulikuwa uamuzi uliofaa. Alinishauri nikomeshe uvutaji sigara kwa muda. Ni yeye tu anayeweza kunishawishi kugura uraibu huu hata ikiwa ni kwa muda wa dakika tano,” akasema Sarri akizungumza na kituo cha habari cha II Mattino.

Mkufunzi huyo amelazimika kutupilia mbali tabia yake hiyo siku za mechi kwa kuwa hairuhusiwi ndani ya viwanja vya soka wakati wa mechi za ligi kuu nchini Uingereza.

Hata hivyo picha zake zilienea mtandaoni akizima kiu chake katika sehemu ya benchi ya kiufundi wakati Chelsea walikuwa wakikabiliana na Newcastle United ugani Stamford Bridge katika mechi ya nne ya EPL.

Ili kufidia uraibu huo, kocha huyo aliye na umri wa miaka 59 amekuwa akitumia sigara bandia wakati wa mechi nne za mwanzo wa msimu kama njia ya kujisahaulisha uraibu huo wakati wa mechi.