Habari Mseto

Niliambia mume kwa nia nzuri kuwa jirani ananitaka, kumbe najipalia makaa!

April 6th, 2024 1 min read

Hujambo shangazi? Mwanamume jirani yetu ameniandama sana akitaka tuwe na mpango wa kando. Nimelazimika kumwambia mume wangu. Sasa anatishia kuniacha akidai nahusiana naye.

Umethibitisha uaminifu wako kwa mume wako kwa kumwelezea kuhusu njama ya jirani yenu. Inashangaza kwamba sasa anakulaumu. Kama hataki kuelewa, itabidi ukubali uamuzi wake.

Kondomu nilizozipata garini zinanitesa moyo

Shikamoo shangazi. Juzi nilipata mpenzi wangu ameficha kondomu ndani ya gari lake. Nimeshindwa kumuuliza kwa sababu najua atanipa sababu za uongo. Waonaje?

Hizo ni dalili kwamba mpenzi wako ana tabia ya kuwinda wanawake wengine na ndiyo sababu anabeba kinga kila wakati. Endelea kuchunguza mienendo yake hadi utakapopata ushahidi.

Mke hataki nilijue dume linalompigia simu za siri

Ninashuku mke wangu ana mpenzi wa pembeni. Kuna mwanamume amekuwa akimpigia simu mara kwa mara na hawezi kuongea naye nikiwa karibu. Nishauri.

Kitendo cha mke wako cha kuwasiliana na mwanamume hiyo kisiri ni dalili kuwa wana uhusiano maalumu. Jaribu upate namba ya mwanamume huyo kisha umpigie umjue.

Sili silali nikiwaza penzi la binti wa bosi wangu!

Mpenzi wangu ni bintiye bosi wangu. Uhusiano wetu umekuwa wa kisiri kwani nilihofia wazazi wake wakijua nitafutwa kazi. Sasa tumeamua kuoana. Tufanyeje?

Si hatia kupendana na binti ya bosi wako. Hatua ambayo mmefikia ni muhimu na itabidi mshirikishe wazazi wenu. Kama mpenzi wako yuko tayari kusimama nawe, huna sababu ya kuwa na wasiwasi.