Nilikataa chanjo ya masonko nikachanjwa ile ya ‘mahasla’ – Kalonzo

Nilikataa chanjo ya masonko nikachanjwa ile ya ‘mahasla’ – Kalonzo

Na SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka sasa amesema alipokea chanjo ya ‘mahasla’ na inayotolewa kwa kila Mkenya. Akionekana kulenga kundi fulani la wanasiasa na mabwanyenye, Bw Kalonzo alisema hakupokea chanjo ya ‘masonko’, kwa kuwa ana imani na ile ya AstraZeneca inayotolewa kwa Wakenya bila malipo.

“Nilipokea chanjo ya AstraZeneca, ya mwananchi. Niliona wengine wakipokea ya Sputnik ya Urusi ya Sh8,000. Ninahimiza Wakenya wajitokeze kuipokea, ili tushinde janga hili la Covid-19,” akasema.

Bw Musyoka alipokea chanjo Jumanne, kufuatia picha alizopakia katika kurasa zake za mitandao ya kijamii. Naibu wa Rais, Dkt William Ruto na mke wake Bi Rachael Ruto pia walipokea chanjo lakini haijabainika alichanjwa Sputnik au AstraZeneca.

Dkt Ruto alisema aliipokea pamoja na familia yake. Akitetea hatua ya kupata chanjo ya AstraZeneca, Bw Kalonzo alisema amepokea majibu ya kuridhisha wengi wakimhakikishia kwamba pia nao watafuata mkondo huo.

“Ninashangaa ikiwa mwananchi anayetegemea wilibaro kusukuma gurudumu lake la maisha atamudu chanjo iliyopokea na ‘wengine’ ya Sh17, 000,” kiongozi huyo wa Wiper akahoji, akiihimiza serikali kuzindua utoaji mkubwa wa chanjo ya AstraZeneca nchini.

‘Wilibaro’ ni kauli ambayo imekuwa ikitumiwa na kundi la Tangatanga linalohusishwa na Dkt Ruto, akisema sera zake hasa akiingia Ikulu 2022 zitakuwa kuinua mwananchi wa kawaida, yaani ‘Hasla’ ambaye mapato yake ni ya kiwango cha chini.

Bw Kalonzo ameitaka serikali kuhakikisha kufikia 2022 imechanja zaidi ya asilimia 30 ya idadi jumla ya Wakenya.

Chanjo ya AstraZeneca na inayoendelea kutolewa nchini ilizinduliwa rasmi Machi 5, 2021 na kuanza kusambazwa Machi 8.

Wahudumu wa afya, maafisa wa usalama na walimu ndio walitangulia. Serikali juma lililopita ilizindua utoaji wa chanjo hiyo kwa wazee waliofikisha miaka 58 na zaidi.

You can share this post!

Kiungo wa Bandari asifiwa na Adebayor

‘One Kenya Alliance haitegemei kumuondoa Raila kwa...