Habari Mseto

'Nilikuja Australia kutazama mbio za magari ya langalanga lakini corona ikanibana'

April 8th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

AUSTRALIA imeshuhudia visa 6,013 vya maambukizi ya virusi vya corona. Kutoka orodha hiyo, 50 wameaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi hivyo.

Mwandishi huyu alipata kuzungumza na Mkenya kwa jina Mwende, ambaye alienda nchini Australia kushabikia mbio za magari ya langalanga zilizofutiliwa mbali mwezi uliopita. Anasema anatamani kurudi Kenya, lakini hawezi kwa sababu Australia imefunga mipaka na pia serikali ya Kenya imeweka vikwazo kama hivyo ili kuzuia uenezaji wa virusi vya corona.

Mwende ameelezea Taifa Leo jinsi ameathirika.

“Inasikitisha unaposhindwa kukutana na rafiki zako kunywa kahawa ama kula nao chakula cha usiku, kuenda katika chumba cha kuona sinema ama hata kula nyama choma na familia na rafiki kwa sababu mikusanyiko ya watu imepigwa marufuku.

Maisha ni magumu sana, hasa kwa wanafunzi na watu ambao stakabadhi zao za visa za kufanya kazi ni za mwaka mmoja; wengi wao ambao wanapatikana katika sekta ya kuandaa vyakula.

Sehemu hizi zimefungwa kumaanisha kuwa hawawezi kufanya kazi. Cha kusikitisha ni kuwa kuna marufuku dhidi ya kusafiri kwa hivyo hawawezi kuenda katika mataifa yao kutafuta usaidizi. Ni maisha magumu sana kwa watu wengine hapa.

Kwa raia wengi wa Australia, mambo yao si mabaya sana kwa sababu karibu asilimia 95 wanaweza kukaa nyumbani na kupokea mishahara yao kwa kati ya asilimia 70 na 80.

Kama tungekuwa na mfumo unaofanya kazi kama wa hapa, tungefaulu nchini Kenya, lakini ukweli ni kuwa Wakenya wengi lazima wafanye kazi mbali na wanakoishi.

Mimi nilikuja hapa Australia kutazama mbio za magari za langalanga mapema mwezi Machi, ambazo hata hivyo zilifutiliwa mbali kabla ya kufanyika.

Kwa bahati nzuri, mimi pia niko na familia hapa na sijatatizika kupata chakula, mahali pa kulala na fedha. Pia, mimi ni mkazi wa visiwa vya Solomon, ambavyo nikitumia ndege kutoka hapa Brisbane ni saa tatu tu na umefika huko.

Kwa hivyo, sijaathirika sana, ingawa nilikuwa nimepanga kuwa nchini Kenya kwa wakati huu, kutatua masuala kadhaa na pia kuona jamaa zangu. Niko hapa nchini Australia kwa visa ya miaka miwili ambayo pia inaweza kuongezwa kwa hivyo sijatatizika sana.”