Habari Mseto

Nilikula uroda na rafiki ya mzee balaa ikatokea, nishauri

February 5th, 2024 1 min read

Mume amekuwa mbali kikazi kwa miaka miwili. Nilishindwa kuvumilia nikashikana na rafiki yake. Sasa nimegundua niko na mimba yake ilhali mzee wangu atarudi hivi karibuni. Nifanyeje?

Shangazi akujibu:

Ndoa na mapenzi ya dhati zinahitaji uvumilivu wa hali ya juu. Wanaoshindwa kuvumilia hujipata katika hali kama yako. Mumeo akifika atajua ukweli. Uwe tayari kwa uamuzi atakaochukua.

Miaka 7 nikimsubiri sasa penzi limeyeyuka

Nimengoja miaka saba ili mpenzi wangu amalize masomo nimuoe. Alimaliza mwaka jana na tunafaa kuanza mipango ya ndoa. Lakini hisia zangu kwake zimepungua sana. Juzi alitaka nimhudumie nikashindwa.

Shangazi akujibu:

Ninashuku hali yako imetokana na mazoea hasa kama mmekuwa mkishiriki tendo la ndoa muda huo wote. Hisia za mapenzi kati ya mume na mke ni nguzo muhimu katika ndoa. Hakuna haja ufunge ndoa ambayo haitadumu. Shauriana na mpenzi wako.

Kumbe anatumia dawa za kuzuia mimba kisiri.

Nina mke na mtoto mwenye umri wa miaka mitano. Tumekuwa tukitafuta watoto zaidi kwa miaka minne bila kufaulu na hatimaye nimejua sababu. Mwenzangu anatumia dawa za kuzuia mimba kisiri.

Shangazi akujibu:

Suala la watoto linahitaji maelewano kati ya mume na mke. Hatua ya mke wako kujizuia kushika mimba bila kukwambia inatia shaka. Zungumza naye ujue kiini halisi ndipo uchukue hatua.

Tulikutana mara moja tu na asema ananipenda

Mwanamume tuliyekutana maskani ya burudani mwaka jana amekuwa akinipigia simu akisema ananipenda. Sina mpenzi lakini pia nashindwa kukubali ombi lake kwa sababu simjui vyema.

Shangazi akujibu:

Huwezi kumpenda mtu ambaye humjui. Kwa kawaida, watu wengi huanza kwa urafiki ili kupima hisia zao. Mwambie unahitaji muda mfahamiane vyema huku ukifikiria kuhusu ombi lake.