HabariSiasa

Nilikuonya, Mutula Junior amkumbusha Ole Kina

February 25th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

SIKU moja baada ya kutetewa na kiongozi wa ODM Raila Odinga, Seneta wa Narok Ledama Ole Kina alitiwa mbaroni Jumanne kwa kutoa matamshi ya uchochezi.

Seneta huyo alikamatwa alipokuwa akitoka kwenye studio za kampuni ya Royal Media Services (RMS) jijini Nairobi alikokuwa amehudhuria mahojiano.

Mnamo Jumatatu, Bw Odinga alimtetea akisema ana haki ya kuzungumzia masaibu yanayokumba jamii yake: “Nimesikia viongozi wakisema kuna matusi hapa na pale, lakini ningependa kuwaambia hiyo ndiyo jinsi ya kuweka msingi bora kwa nchi hii. Hakuna mtu amekatazwa kusema jambo lolote linalomkera pamoja na jamii yake. Acheni kila mtu atapike nyongo na azungumze kwa uwazi ili tujenge Kenya mpya.”

Bw Ole Kina alinaswa na maafisa wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) na kupelekwa katika Kituo cha Polisi kuhojiwa.

Tume ya Maridhiano na Utangamano (NCIC) ilithibitisha kuwa ilishirikiana na maafisa wa DCI kumnasa seneta huyo anayedaiwa kutoa matamshi ya chuki wakati wa mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini.

Maafisa wa DCI walipowasili katika afisi za RMS walimtaka Ole Kina kuabiri gari walilokuwa nalo. Lakini alikataa akisisitiza angetumia gari lake.

Maafisa wa DCI walimshinikiza kushuka. Aliposhuka kutoka kwenye gari lake na kuingia gari la maafisa wa DCI, seneta huyo alikataa kuketi katikati ya maafisa wawili wa polisi akidai kuwa wangemchafulia koti lake.

“Siwezi kuketi katikati kwa sababu mnanichafulia koti langu. Mniruhusu nivue koti ndipo niketi katikati,” akasema.

Maafisa wa DCI walimruhusu kushuka ndipo akavua koti na kulikunja vizuri kabla ya kuingia ndani ya gari na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kilimani.

Muda mfupi baada ya kukamatwa, Bw Ole Kina aliandika kwenye mtandao wa Twitter: “Nimekamatwa sasa hivi” na badala ya kuhurumiwa, baadhi ya maseneta wenzake walianza kumkejeli.

Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja alimjibu kwa kusema: “Lakini unaonekana mwenye furaha”.

Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior alisema: “Unaonekana kushangaa. Unakumbuka nilivyokuonya hivi karibuni?”

Seneta wa Elgeyo- Marakwet Kipchumba Murkomen alisema: “Ninashangaa ikiwa inafaa kukamata watu kama Seneta Ledama Ole Kina.

Nimesema hapa mara kadhaa kwamba watu kama Ole Kina wapelekwe kwenye makao ya kubadili tabia kwani wanajaza seli bure.”

Akiwa seli alirekodi video na kuitia katika mitandao ya kijamii akiapa kuendelea kupigania haki ya jamii ya Wamaasai.

Bw Ole kina amejitokeza kuwa mtetezi wa jamii ya Wamaasai huku akidai wanapokonywa ardhi yao na watu kutoka nje ya kaunti hiyo.

Amekuwa akisisitiza kuwa wageni wamekuwa wakinunua ardhi kwa chini ya Sh70,000 katika maeneo yaliyo na Wamaasai wengi kama vile Narok na Kajiado na kisha kuiuza kwa bei ya juu.