Habari Mseto

Nilikupenda sana, mke wa jasusi wa NIS aliyejitoa uhai asema akimwomboleza

June 14th, 2024 1 min read

NA RUSHDIE OUDIA

MKE wa afisa wa ujasusi Tom Adala anayedaiwa kujiua kwa kujipiga risasi nyumbani mwake amemuomboleza kama rafiki, msiri wake na mshirika katika maisha yao ya ulezi wa watoto wao.

Ripoti ya polisi inasema Bw Adala alijiua nyumbani kwake katika makazi ya Kirichwa Villas, Kilimani kutokana na kuugua shinikizo la mawazo.

Makachero waliozuru eneo la mkasa walibaini kwamba jamaa huyo aliyekuwa na umri wa miaka 54 alijiua kwa kutumia bastola usiku wa Jumanne, Juni 4, 2024.

Bw Adala alikuwa Naibu Mkurugenzi katika Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) ambayo makao makuu yake ni Ruaraka, Nairobi.

Kifo chake kimetajwa na jamaa na marafiki waliozungumza na Taifa Leo kuwa kilitokana na msongo wa mawazo kutokana na shinikizo za kikazi pamoja na matatizo ya ndoa.

Haya yaligusiwa pia kwenye barua anayodaiwa aliacha baada ya kujitoa uhai.

Lakini siku chache kabla ya mazishi yaliyopangiwa kufanyika Juni 15, mkewe amemmiminia sifa kedekede kwa mara ya kwanza, akigusia kuhusu ‘mashaka’ mumewe alikuwa akikabiliana nayo.

Akimwita ‘Tom’, Bi Habiba Seby alijieleza kwa kirefu kwenye wasifu alioandika na uliochapishwa kwenye kitabu cha maombolezo, chenye kichwa, ‘Urithi wa Mapenzi’.

“Kwa kukukumbuka, sote tutafahamu mashaka ya kibinafsi wengine wanapitia. Ingawa hupo hapa nasi, tunahisi uwepo wake katika kila jambo tunalofanya,” akaandika Bi Seby.

Anaendelea kusema kwamba kifo cha Adala kimemwathiri mno na kwamba kimeacha pengo kubwa kwenye maisha yao kama familia.

Kulingana na Bi Seby, Adala alikuwa mwenye tabasamu kila mara, mwenye maneno ya kutia moyo, aliyeshiriki nyakati na watu na kuwatia shime na nguvu, pamoja na ukarimu.

Anasema laiti mumewe angefahamu jinsi alivyopendwa na watu wengi kwa sababu alikuwa na uwezo wa kuonyesha mapenzi kwa kila aliyetangamana naye.

“Nitaendelea kukuweka moyoni mpaka siku tutakapoonana tena,” akahitimisha.