Dondoo

Nilikuwa nataka mtoto tu, mke amwambia polo baada ya kumtema

June 12th, 2019 1 min read

Na Ludovick Mbogholi

KIMBUNGA KASHANI, Mombasa

POLO wa hapa alijipata matatani kwa kuumbuliwa peupe na demu aliyemuoa miaka miwili iliyopita baada ya kujifungua mtoto.

Yasemekana demu alimweleza jamaa kuwa hakuwa na haja ya ndoa bali alikuwa akitaka mtoto tu. “Demu aliolewa miaka miwili iliyopita, lakini aliposhika mimba alianza kubadili tabia,” alisema mdaku wetu.

Kulingana na mdokezi kabla ya kupata mimba, alikuwa akimpenda sana mumewe, mara kwa mara waliandamana naye kwenye maduka kununua bidhaa. Aliposhika mimba, tabia ilibadilika kabisa. “Hakutaka jamaa amuulize lolote, na akiulizwa alijibu kwa ujeuri,” alieleza mdaku.

Mwanzo polo alidhani mkewe alikuwa akisumbuliwa na uja uzito, lakini alipojifungua alishuku alikuwa na jambo aliloficha moyoni mwake kwani alizidisha ujeuri. Ilibidi jamaa amuulize kilichokuwa kikiendelea na jibu alilopata lilimuumiza moyo.

“Haja yangu ilikuwa kupata mtoto tu. Sina haja na wewe na ukome kunisumbua,” demu alimjibu kwa dharau. Jamaa alipandwa na za kwao na kumuuliza demu kwa nini alikubali amuoe. “Kwanini hukunikataa nilipokuoa tuachane mapema ila ulipojua una mimba ukaanza kuniletea vituko?” polo alifoka.

“Nilitaka unitunze nikiwa na mimba, ikomae halafu nijifungue salama, sasa nimejifungua. Sina haja nawe,” demu aliropokwa maneno ya kumdhalilisha polo.

Kulingana na mdokezi, demu alimfanyia polo vituko kabla ya kumuacha.

“Acha aende, mtoto akiwa mkubwa atamtafuta babake, vituko alivyonionyesha vinatosha,” polo alisikika akisema.