Habari

Nililipwa Sh700,000 kusafiri ng’ambo na Mandago, afisa afichua

Na JOSEPH OPENDA July 2nd, 2024 2 min read

AFISA mmoja wa Kaunti alishangaza Mahakama ya Nakuru baada ya kukiri kupokea kitita cha hela kwa kuandamana na aliyekuwa Gavana waUasin Gishu Jackson Mandago, kusafiri ng’ambo 2021.

Mwenyekiti wa Hazina ya Maendeleo wa Kaunti ya Uasin Gishu, Joel Cheruiyot Chelule, alieleza mahakama kuwa alilipwa Sh700,000 kama masurufu ili kuandamana na aliyekuwa bosi wake wakati huo katika mataifa ya Finland na Canada, ili kutia saini Mkataba baina ya vyuo vikuu vitatu, unaohusu elimu ya ng’ambo kwa wanafunzi kutoka humu nchini.

Afisa huyo alitoa ushahdi katika kesi ambapo Bw Mandago, ambaye ndiye sasa Seneta wa Uasin Gishu na maafisa wawili, Joshua Lelei na Meshack Rono, wameshtakiwa kuhusu sakata ya Sh1 bilioni za ufadhili wa elimu.

Hata hivyo, alieleza mahakama kwamba hakufahamu wajibu wake katika ziara hiyo wala kuelewa sababu ya kujumishwa kwake.

Ziara hiyo ilichukua muda wa siku tisa kati ya Agosti 12 na Agosti 21, 2021.

Miongoni mwa waliokuwepo katika ziara hiyo ni gavana, msaidizi wake binafsi na maafisa wa kaunti wakiwemo Joel Ruto na Joseph Maritim.

“Tiketi za Finland na Canada zililipwa na Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu na nilipokea takriban Sh 700,000 za masurufu kutoka kwa kaunti. Sikujua kusudi la kunijumuisha miongoni mwa wajumbe hao na nilifikiri gavana alitaka niwe sehemu ya timu hiyo kushuhudia mkataba huo ukitiwa saini,” alisema Bw Cheruiyot.

Madai ya Bw Cheruiyot yalifanya timu ya mawakili wanaotetea washtakiwa kuhoji iwapo alikwenda ziara hiyo kujivinjari tu.

Isitoshe, shahidi huyo alikana kuwa alisafiri kama mwenyekiti wa Hazina ya Elimu Uasin Gishu.

Alikana vilevile kufahamu kuhusu kuwepo hazina hiyo akisema alijua kuihusu baada ya ziara hiyo Septemba 2022.

Hii ni baada ya kuagizwa na waziri wa elimu kaunti hiyo kujibu malalamishi yaliyowasilishwa na wazazi wakitaka kujua hatima ya watoto wao baada ya kulipa hela za mradi huo wa ng’ambo.

Bw Cheruiyot alisema aliitwa na waziri wa elimu aliyemfahamisha kuwa wanachama wa Hazina ya Elimu ya Ng’ambo Uasin Gishu, ambayo alikuwa mmoja wao, ndio pekee wenye uwezo wa kujibu malalamishi hayo.