Michezo

Nilimtandika Zarika lakini majaji wakampa ushindi – Mercado

September 12th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

MWANABONDIA kutoka Mexico Yamileth Mercado ambaye alipoteza vita dhidi ya Mkenya Fatuma Zarika sasa amelaumu majaji wa pigano hilo kuwa walimwonea.

Mercado alishindwa kwenye pigano hilo la Jumamosi katika uwanja wa kimataifa wa KICC.

Jaji Eddie Papoe wa Ghana alimpa Mercado pointi 96-94, huku wa Kenya Bena Kaloki na Francis Chirwa kutoka Malawi wakimpa Zarika 97-93 na 99-91 katika pigano hilo la raundi kumi kupigania taji.

Baadaye, Mercado alizungumza kupitia mtandao wake wa Twitter, akilalamika kuwa alionewa lakini akakiri kuwa alifurahishwa na Wakenya kujitolea kuhudhuria.

Yamileth Mercado @YeimiMercado16 “Asante Kenya, nimekasirishwa na hatua ya majaji kuegemea upande wa Zarika, lakini niliridhishwa na watu wake (Kenya) nilikaa vizuri.”

Mwanabondia huyo wa Mexiko sasa aliongeza kushindwa mara moja kwenye rekodi yake ambayo mbeleni ilikuwa mapigano 13, yakiwa na ushindi wa mapigano 12 na kushindwa mara moja.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo mbeleni, alionya kuwa watu wasidanganywe na sura yake ya usichana wakadhani hataweza vita.

Alikuwa mkakamavu kuwa mazoezi aliyopiga yangemsaidia kumnyanganya Zarika taji la baraza la uanadondi duniani (WBC) kuwa mwanamke hatari zaidi katika mchezo huo.