HabariSiasa

Nilimteua Miguna kuzima presha – Sonko

May 28th, 2018 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

GAVANA wa Nairobi, Mike Sonko amesema uamuzi wake wa kumteua wakili mbishi Miguna Miguna kuwa naibu wake ulichochewa na presha ambayo amekuwa nayo kutoka kwa baadhi ya maafisa wa juu katika serikali kuu.

Gavana Sonko, aliyekuwa akizungumza kwa mara ya kwanza mara baada ya kurejea jijini Nairobi kutoka nyumbani kwake katika Kaunti ya Machakos, alikoenda kutokana na kisingizio kwamba maisha yake yalikuwa hatarini, alisema viongozi wa ngazi za juu serikalini walikuwa wakimshinikiza kuteua wandani wao kuwa naibu wake.

“Nimesumbuliwa na makatibu wa wizara, mawaziri na watu wafisadi serikalini. Kila mtu alikuja na mtu wake akiniambia Sonko chagua huyu, katibu wa wizara anakwambia chagua huyu naye waziri anakwambia chagua huyu, ilhali rais mwenyewe hajasema kitu,” akasema Bw Sonko aliyekuwa akizungumza katika kanisa la African Independent Pentecostal Church (AIPCA) katika eneo la Njiru, eneobunge la Kasarani.

Gavana Sonko alisema alimteua Dkt Miguna ili kunyamazisha baadhi ya maafisa wa ngazi ya juu serikalini.

“Mimi nilipoona wakinisumbua nilisema potelea mbali! Wacha Miguna ambaye alinitukana aje awe naibu wangu anisaidie kupigana na hao watu katika Jumba la Harambee,” akaongeza.

“Nilijua hiyo ndiyo dawa ya kuwaweza hao maafisa walio katika Jumba la Harambee kwa sababu wao ndio walimpa Dkt Miguna paspoti na kitambulisho cha kitaifa na hata wakamuidhinisha kuwania ugavana katika uchaguzi wa Agosti 8 mwaka 2017,” akaongezea.

Gavana Sonko, aliyekuwa ameandamana na baadhi ya madiwani na mawaziri wake, alisema uamuzi wa kuidhinisha au kukataa jina la Dkt Miguna uko mikononi mwa Bunge la Kaunti ya Nairobi.

Baadhi ya viongozi wa Jubilee wakiongozwa na naibu mwenyekiti David Murathe wamekuwa wakishinikiza kutimuliwa kwa Bw Sonko kutokana na kigezo kwamba ameshindwa kutekeleza majukumu yake.

Lakini Jumapili, gavana huyo aliwashambulia wanaoshinikiza atimuliwe akisema madiwani wana imani na uongozi wake.

Kwa wiki moja Bw Sonko amekuwa akiendeshea shughuli za serikali ya Kaunti ya Nairobi nyumbani kwake katika eneo la Mua Hills, Kaunti ya Machakos akidai kwamba maisha yake yako hatarini baada ya kupunguziwa walinzi hadi watano.

Alisema kuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga ni miongoni mwa viongozi ambao walimpigia simu wakimtia moyo wa kuendelea kuhudumu bila uwoga.

“Napenda kumshukuru aliyekuwa Waziri Mkuu Bw Odinga kwa kunipigia simu akiniambia kuwa niwe imara na wala nisibababaike,” akasema Gavana Sonko.