Kimataifa

Nilimuua mume wangu kwa kutesa paka wangu, akiri mwanamke

June 11th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

DALLAS, AMERIKA

WAKAZI wa eneo la Dallas walishtushwa na jinsi mwanamke alivyokiri kwamba alimuua mume wake kwa kuwa alikuwa anampiga paka wao.

Ripoti zilisema Mary Harrison, 47, alikamatwa na kushtakiwa kwa kumuua mume wake, Dexter Harrison, 49.

Ilisemekana aliambia polisi kwamba mume wake alikuwa akimpiga paka wao wa nyumbani ndipo akampiga risasi na kumuua.

“Alisema walibishana kuhusu kwa nini mume wake alikuwa akimpiga paka na hapo ndipo akampiga risasi na kumuua,” polisi walinukuliwa kusema.

Mwanamume huyo alikimbizwa hospitalini lakini akathibitishwa kufariki, na mshukiwa akaenda katika makao makuu ya polisi eneo hilo ambako alihojiwa na wapelelezi wa jinai.

“Wakati alipohojiwa, alikiri kutekeleza kosa hilo akakiri kwamba alimpiga mwathiriwa risasi,” mashirika yalizidi kunukuu polisi.

Majirani waliohojiwa na wanahabari walisema paka huyo alikuwa amepotea hivi majuzi lakini akarejea nyumbani baadaye. Wakati paka alipokuwa ametoweka, ripoti zinasema mwanamke huyo alibandika picha zake katika sehemu mbalimbali mtaani ili kutangaza yeyote ambaye angemwona amrudishe nyumbani.

-Imekusanywa na Valentine Obara