Michezo

Nilimwachia Rashford apige penalti dhidi ya Basaksehir – Bruno Fernandes

November 25th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KIUNGO Bruno Fernandes wa Manchester United amesema kwamba alikataa fursa ya kufunga mabao matatu dhidi ya Basaksehir ya Uturuki kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 24, 2020, baada ya kumwachia mwenzake Marcus Rashford kuuchanja mkwaju wa penalti.

Baada ya kufunga mabao mawili katika dakika za saba na 19 na kuwaweka Man-United kifua mbele kwa 2-0 chini ya dakika 20 za kipindi cha kwanza, Fernandes aliyefunga penalti dhidi ya West Brom katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) siku tatu zilizopita, alikataa fursa ya kuchanja penalti dhidi ya Basaksehir na badala yake kumwomba Rashford afanye hivyo na kufanya mambo kuwa 3-0.

“Bila haka kila mchezaji hutaka fursa ya kufunga mabao matatu katika mechi moja. Lakini baada ya kufunga penalti dhidi ya West Brom katika mechi ya awali, tena baada ya jaribio la kwanza kupanguliwa na kipa, niliona vyema Rashford apige mkwaju huo uliopatikana dhidi ya Basaksehir,” akasema sogora huyo raia wa Ureno.

“Isitoshe, Rashford ni miongoni mwa wafungaji bora wa UEFA kufikia sasa. Hivyo, ilikuwa vyema afunge bao dhidi ya Basaksehir ili azidi kujiamini,” akaongeza Fernandes kwa kukiri kwamba haijalishi nani atapiga penalti kambini mwa Man-United kwa sasa bora tu kikosi kifunge na kushinda mechi.

“Rashford ni mzuri pia katika kupiga penalti. Sikuwa na tatizo kabisa baada ya Fernandes kuteua kumpa mkwaju dhidi ya Basaksehir. Anthony Martial pia ni mzuri sana na aliwahi kufunga moja dhidi ya Leipzig. Huo ndio ushirikiano tunaohitaji kikosini,” akasema kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Mechi dhidi ya Basaksehir ilikuwa ya kwanza kuwahi kushuhudia Man-United wakiongoza kwa mabao matatu kwa bila katika UEFA ugani Old Trafford tangu wafanye hivyo katika ushindi wa 7-1 dhidi ya AS Roma ya Italia mnamo Aprili 2007.

Basaksehir walifutiwa machozi na fowadi Deniz Turuc katika dakika ya 75 kabla ya Daniel James kufunga la nne kwa upande wa Man-United mwishoni mwa kipindi cha pili.

Man-United kwa sasa wameshinda mechi saba zilizopita za soka ya bara Ulaya kwa jumla ya mabao 24-2. Kwa upande wao, Basaksehir wamepoteza michuano minne iliyopita ugenini kwenye bara Ulaya kwa kufungwa mabao 12 nao wakipachika wavunia magoli mawili pekee.

Man-United kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Southampton kwenye EPL uwanjani St Mary’s mnamo Novemba 29, 2020.