Habari MsetoSiasa

Niliogopa sana kupoteza 'bedroom yangu' Kibra – Raila

November 11th, 2019 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

KINARA wa ODM Raila Odinga amefichua kuwa alikuwa na hofu ya kubwagwa na Naibu wa Rais William Ruto katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kibra.

Bw Odinga alielezea namna wakazi wa Kibra walimwokoa kutokana na aibu ambayo angepata iwapo mwaniaji wa Jubilee McDonald Mariga angemshinda mwaniaji wa ODM Benard ‘Imran’ Okoth katika uchaguzi mdogo uliofanyika Alhamisi iliyopita.

Bw Okoth aliibuka mshindi baada ya kupata kura 24,636 huku Bw Mariga akifuatia kwa kura 11,230. Eneobunge la Kibra lina jumla ya watu 118,658 waliojiandikisha kupiga kura.

Bw Odinga alifichua kwamba idadi ndogo ya watu waliojitokeza kupiga kura ilitia tumbojoto viongozi wa ODM pamoja wanasiasa wa Kieleweke.

“Nilikuwa nyumbani kwangu nikifuatilia matukio lakini kilichotia hofu baadhi ya viongozi ni idadi ndogo ya watu waliojitokeza kupiga kura,” akasema Bw Odinga.

Akaendelea: “Ilibidi tutume vijana waende kupiga firimbi na kuzunguka mtaani Kibra wakisema ‘bedroom’ (chumbani), ‘bedroom’ (chumbani), ndipo watu wakajitokeza kupiga kura.”

Bw Odinga alikiri kwamba kushindwa kwa ODM katika uchaguzi mdogo wa Kibra kungeathiri mchakato wa kutaka kubadili Katiba kwa kuzingatia ripoti ya jopo maalumu lililobuniwa kukusanya maoni kuhusu namna ya kuunganisha Wakenya, maarufu BBI.

“Uchaguzi mdogo wa Kibra ulikuwa wa manufaa kwa taifa zima na wala si kwa Wanakibra pekee. Asante sana kwa kuniondolea aibu,” akasema Bw Odinga aliyekuwa akizungumza katika mkutano wa shukrani ulioandaliwa katika Uwanja wa DC mtaani Kibra.

Mkutano huo wa shukrani ulihudhuriwa na Magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Alfred Mutua (Machakos) na Naibu Gavana wa Kiambu James Nyoro.

Viongozi wa kundi la Kieleweke waliongozwa na wabunge Maina Kamanda (Maalumu), Joshua Kuttuny (Cherangany) na aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Kusini Dennis Waweru. Bw Kamanda aliwasili uwanjani hapo kwa kutumia helikopta kutoka Kaunti ya Nyandarua alipokuwa amehudhuria ibada ya kanisa.