Nilipokuwa Naibu Rais kazi bora ilifanyika – Ruto

Nilipokuwa Naibu Rais kazi bora ilifanyika – Ruto

Na SAMMY WAWERU

NINAHESHIMU uamuzi wa Rais Uhuru Kenyatta kunivua kofia la majukumu yangu kama msaidizi wake, Naibu Rais William Ruto sasa amesema.

Dkt Ruto amesema awamu ya kwanza wakati alikuwa akishirikiana na kiongozi wa nchi kazi waliyofanya ilikuwa bora na ya kupigiwa upatu.

“Wakati nilikuwa naibu wa rais anayetambulika, ndipo tulizindua mradi wa reli ya kisasa (SGR), taasisi za elimu ya juu na ujenzi wa barabara. Nilichangia pakubwa kutekeleza miradi ya maendeleo tunayojivunia sasa.

“Baada ya 2017, niliambiwa nikae kando kuna wengine watafanya majukumu yangu,” akasema Naibu Rais, akilalamikia kutengwa katika serikali tawala ya Jubilee.

“Kazi niliyokuwa nikitekeleza ninaona inafanywa na Waziri Fred Matiang’i (Usalama wa Ndani na Mikakati ya Serikali),” akasema.

Dkt Ruto alitoa matamshi hayo Jumatano, kwenye mahojiano na runinga ya Inooro, inayopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kikuyu.

“Watu wengi wanashangaa kwa nini sera ninazotumia kuomba kuwa rais 2022, zisizitumii serikalini. Wakenya wanajua nilipokuwa nasaidia Rais, kazi bora ilifanyika,” akasema.

“Kati ya marais watatu wa kwanza (Mzee Jomo Kenyatta, Daniel Arap Moi na Mwai Kibaki), Mzee Kibaki ametajwa kuwa bora zaidi. Alipokuwa makamu wa rais wa Mzee Moi, hakukosolewa, alipochukua hatamu ya uongozi alichapa na kuacha rekodi bora. Ninapoomba kuwa rais 2022 nina uhakika na utendakazi wangu,” akafafanua.

Alitumia mfano wa Wizara ya Elimu na Kilimo, wakati wa utawala wa serikali ya mseto, iliyoongozwa na Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki na Raila Odinga akiwa Waziri Mkuu, akihoji alisaidia kuziimarisha.

You can share this post!

Ndugu wawili wakana kuibia Benki ya Dubai Sh154milioni

Siwezi kufanya kazi na Raila, Ruto asema