Shangazi Akujibu

Nilishangaa mpenzi hataki tuonane usiku, kumuuliza akasema yeye huchuuza asali

February 27th, 2024 1 min read

SHANGAZI,

Nimekuwa nikishangaa kwa nini mpenzi wangu hawezi kukubali tukutane usiku. Ameungama kuwa yeye ni kahaba na huwa kazini. Ameniomba msamaha na kuahidi kuacha kazi hiyo. Nishauri.

Mpenzi wako amekwambia ukweli na yuko tayari kuacha kazi hiyo kwa sababu yako. Kama unampenda msaidie kufungua ukurasa mpya wa maisha yake.

Amenizimia simu tangu nijue ana mwingine

Mpenzi wangu anaishi mbali. Juzi nilipata habari kuwa ana mwingine na nilipomuuliza kwa simu akakana. Nilimuomba tukutane ili tuzungumze. Lakini tangu siku hiyo amenifungia simu siwezi kumpigia. Nifanyeje?

Kuna uwezekano mkubwa kwamba habari hizo ni za kweli. Ingawa mpenzi wako alikana kwa simu, anahofia una ushahidi na anaogopa kwamba mkikutana atashindwa kujitetea. Achana naye.

Nahofia akijua nimeavya mimba nyingi hatanioa

Mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka miwil anataka kunioa. Lakini nahofia uwezo wangu wa kupata watoto kwa sababu nimeharibu mimba nyingi tena za wanaume wengine.

Sielewi kwa nini hukutumia kinga kuepuka mimba hizo. Kama hutaki matatizo baada ya ndoa, muone daktari wa afya ya uzazi akupime ili ujue hali yako. Matokeo yakiwa mabaya utajilaumu.

Sweet mama balaa tupu, haambiliki hasemezeki!

Nimependana na mwanamke aliye na miaka 45. Shida iliyopo ni kwamba haamini ninaweza kumpa ushauri wowote wa maana kwa sababu amenizidi kwa umri na pesa.

Mume ndiye kiongozi wa familia na nastahili kuheshimiwa na kupewa nafasi ya kutoa mwelekeo wa maisha ya familia yake. Kama mpenzi wako hawezi kutambua nafasi yako hiyo katika ndoa, ni heri muachane.