HabariHabari MsetoSiasa

Nilishtuka mno kuamshwa na watu wakisaka ushahidi kwa nyumba yangu – Waiguru

August 20th, 2020 1 min read

Na MARY WANGARI

Gavana wa Kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru yamkini amekerwa baada ya makachero wa EACC kuvamia makao na afisi yake mapema Alhamisi, Agosti 20, 2020.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, bosi huyo wa kaunti alitaja kisa hicho kama njama za kisiasa zinazochochewa na siasa za urithi katika eneo la Mlima Kenya.

Kulingana naye, kisa hicho kililenga kuwafumba macho Wakenya ili waache kuuliza maswali kuhusu uporaji uliokithiri wa mali ya umma katika siku za hivi karibuni.

“Hizi ni njama zilizodhamiriwa kuwatatiza watu ambao hivi majuzi wamekuwa wakiuliza maswali ya haki kuhusu jinsi kiasi kikubwa cha fedha za umma kimekuwa kikitumika,” ilisema taarifa.

Gavana huyo alisisitiza kwamba kwa mara nyingine, alikuwa akitumiwa kama chambo huku akisema kuwa njama hizo zitagonga mwamba sawa na jinsi zilivyokosa kufaulu hapo awali.

“Nimekuwa hapa hapo mbeleni. Nimetumika kama chambo mbeleni. Njama hizo zilifeli na zitafeli hata sasa. Madai yasiyo na msingi yanarushwa kiholela na kuambulia patupu bila hata ushahidi thabiti. Huu ni mtego,” alisema.

Kiongozi huyo alishangaa ni kwa nini EACC ililazimika kutuma kundi la makachero waliojihami katika uvamizi huo alfajiri ili kutwaa tu kitabu cha hundi ilhali angekiwasilisha kirahisi endapo angehitajika kufanya hivyo.

“Hivyo basi hakuna chochote unachoweza kutafuta katika nyumba ya mtu kama ushahidi wa usimamizi wa matumizi. Ni jambo la kushtusha kuamshwa na kundi la maafisa waliojihami kikamilifu wakivamia nyumba yangu kutafuta ushahidi kuhusu hela za matumizi.

“Kwa hakika, hukuhitaji kikosi cha maafisa wa polisi waliojihami kwa bunduki, kuvamia boma langu gizani ili kutwaa kitabu cha hundi! Kingepatikana kupitia agizo rahisi tu,” alihoji.

Waiguru alieleza kuwa tayari alikuwa amewasilisha stakabadhi husika wakati wa kikao cha Seneti kuhusu jaribio la kumng’atua mamlakani, kilichopeperushwa moja kwa moja kupitia vituo vya televisheni.

Aidha, alisaili kuhusu mabadiliko katika kiasi cha hela alizohusishwa nazo katika kikao hicho cha Seneti mnamo Mei kutoka Sh22 milioni hadi Sh10 milioni.