Habari Mseto

Nilistaafu NMG kwa hiari yangu, asema Lolani Kalu

October 2nd, 2020 1 min read

Na HASSAN MUCHAI

MWANAHABARI na msanii Lolani Kalu, amekanusha habari ambazo zimekuwa zikienea kupitia mitandao ya kijamii kwamba alifurushwa kazi na kampuni ya Nation Media Group.

Baada ya habari zake kuangaziwa kwenye makala ya ‘Mshairi wa Wiki’ katika gazeti la Taifa Jumapili mwezi uliopita, mashabiki wake wamekuwa wakitamaushwa na picha za kuhuzunisha ambazo zimekuwa zikionyeshwa mitandaoni zikimwonyesha amedhoofika kiafya.

Kwenye mahojiano na wanahabari waliomtembelea jana nyumbani kwake eneo la Kaloleni-Giriama, Bw Kalu alisisitiza kuwa aliacha kazi kwa hiari.

Alisema kuwa ana uhusiano mzuri sana na NMG na amekuwa akiwasiliana na shirika hilo kila anapotaka.

Hata hivyo, alisema amekuwa akipitia kipindi kigumu cha maisha baada ya kumpoteza babake mzazi mara tu baada ya kuacha kazi.

Zaidi ya hayo, amekuwa akimuuguza mamake mzazi wa miaka 90 licha ya kuwa hana kazi.Kwa mujibu wa Bw Kalu, masaibu yake yalianza punde tu alipoacha kazi kwa kulaghaiwa zaidi ya Sh1.5 milioni na mjenzi aliyemuahidi kumsaidia kujenga makao yake eneo la Kangundo.

‘Nilimwamini sana mwekezaji huyo. Nimekuwa nikimfuatilia bila mafanikio. Hata laini yake ya simu ameizima,’ alisema.

Alieleza matumaini ya kumaliza ujenzi wa kituo cha maonyesho ya utamaduni na sanaa nyinginezo cha Zamila kilichokwama mara tu baada ya kisa cha ugonjwa wa corona kuripotiwa nchini.Mbali na NMG, Bw Kalu aliwahi pia kufanya kazi katika shirika la KBC.