Habari za Kitaifa

Nilitumia Sh10m pekee kwa ziara ya Amerika – Ruto

May 30th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto sasa amefafanua kwamba ni Sh10 milioni pekee, pesa za umma, zilizotumika kugharimia ukodishaji wa ndege ya kibinafsi na ya kifahari aliyotumia katika ziara yake nchini Amerika.

Akiongea Alhamisi asubuhi wakati wa Maombi ya Kitaifa katika mkahawa wa Safari Park, Dkt Ruto alisema kiasi kingine cha pesa zilizotumika kugharimia ukodishaji wa ndege, zilitolewa kama msaada kutoka kwa marafiki wa Kenya ambao hakuwataja.

“Nilipouliza kuhusu gharama ya kukodisha ndege hiyo, niliambiwa ni Sh70 milioni. Lakini nikawaambia siko tayari kutumia zaidi ya Sh10 milioni. Hapo ndipo marafiki zangu waliingilia kati na kulipa pesa zilizosalia,” akaeleza.

Hata hivyo, hakuwataja marafiki hao waliojitolea kuchangia gharama ya safari yake.

Rais Ruto alisema kuwa yeye kama Rais anapaswa kuwa katika mstari wa mbele kupunguza gharama ya matumizi serikalini na hivyo, katu hawezi kutumia pesa nyingi kupita kiasi kugharimia safari zake za ng’ambo.

“Mimi si mwendawazimu wa kuwaambia wananchi kwamba serikali inapunguza gharama kisha nigeuke mbadhirifu. Ninaoongoza kutoka mbele katika mpango huu wa utekelezaji mikakati ya kupunguza gharama na ninaahidi kuwa ndani ya miaka mitatu ijayo, tutakuwa na bajeti iliyosawazishwa. Hatutaki bajeti ambayo utekelezaji wake unaanza kwa serikali kukopa kutoka nje,” Dkt Ruto akasema.

Rais aliwamba Wakenya kukomesha mjadala kuhusu gharama ya ukodishaji wa ndege ya kibinafsi aliyotumia kwa safari yake nchini Amerika.

Wiki jana, Wakenya wa tabaka mbalimbali walilalamika ilipofichuka kuwa Rais Ruto na ujumbe wake, walitumia ndege ya kibinafsi na kifahari aina ya Boeing 737-700 inayomilikiwa na kampuni ya Royal Jet ya Dubai inayogharimu Sh98 milioni kwa safari ya kwenda Amerika pekee.

Ikakadiriwa kuwa serikali ilitumia karibu Sh200 milioni kwa kugharimia safari ya kuenda Amerika na kurudi Kenya kwa kutumia ndege hiyo.

Hiyo ni kando na gharama nyingine kama vile ndege hiyo kumsibiri Dkt Ruto kwa muda wa siku nne, gharama ya ndege hiyo kusafiri kutoka Dubai hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kumbeba na rubaa yake na tena kurejea Dubai baada ya ziara hiyo kufikia kikomo.

Aidha, pesa za mlipa kodi zilitumika kugharimia malazi, chakula, marupurupu na matumizi mengi ya ujumbe wa maafisa wa serikali na wanasiasa, wakiwemo wa Azimio La Umoja-One Kenya, walioandamana na Rais Ruto katika ziara yake ya Amerika.

Mapema wiki hii, vinara wa Azimio wakiongozwa na Makamu wa Rais wa zamani Stephen Kalonzo Musyoka, walimpapura vikali Rais Ruto kwa kile walidai alifanya ubadhirifu wa pesa za umma wakati wa ziara yake ya Amerika.

“Haijalishi manufaa ambayo ziara ya Rais itailetea Kenya, Sh200 milioni si pesa kidogo. Huu ni ubadhirifu wa pesa za umma,” Bw Musyoka akasema alipotembelea soko la Gikomba, Nairobi kuwapa pole wafanyabiashara ambao vibanda vyao vilibomolewa na serikali kwa kujengwa karibu zaidi na Mto Nairobi.