Niliwahi kujaribu kumsajili Bruno Fernandes wa Manchester United nikiwa kocha wa PSG – Tuchel

Niliwahi kujaribu kumsajili Bruno Fernandes wa Manchester United nikiwa kocha wa PSG – Tuchel

Na MASHIRIKA

KOCHA Thomas Tuchel amemsifia kiungo Bruno Fernandes kwa ukubwa wa ushawishi wake uwanjani kila anapovalia jezi za Manchester United na kufichua kwamba aliwahi kuwa pua na mdomo kujinasia huduma za mwanasoka huyo raia wa Ureno wakati akidhibiti mikoba ya Paris Saint-Germain (PSG).

Kufikia sasa, Fernandes amefungia Man-United jumla ya mabao 34 kutokana na mechi 60 na anatarajiwa kuwa tegemeo kubwa kambini mwa mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika mechi itakayowakutanisha na Chelsea mnamo Februari 28, 2021 uwanjani Stamford Bridge.

Tuchel anasema kwamba alimfahamu Fernandes kwa mara ya kwanza mnamo 2018 kupitia kwa aliyekuwa mkurugenzi wa michezo kambini mwa PSG, Antero Henrique.

“Tulijaribu kumsajili mnamo 2018 japo juhudi zetu hazikuzaa matunda. Nilikuwa nimekubali tu kudhibiti mikoba ya PSG na Henrique akanitajia kuhusu mchezaji huyo aliyekuwa akimfuatilia sana. Tulitazama mechi nyingi alizocheza sogora huyo na tukaanza mchakato wa kumsajili baada ya kuridhishwa na mchezo wake,” akafunguka Tuchel aliyehudumu kambini mwa PSG kati ya 2018 na 2020.

Bruno Fernandes (kulia). Picha/ AFP

Baada ya kukataa ofa ya PSG, Fernandes, 26, alihiari kutua ugani Old Trafford kuvalia jezi za Man-United waliomsajili kutoka Sporting Lisbon ya Ureno mnamo Januari 2020.

Kwa mujibu wa Tuchel ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Borussia Dortmund, Fernandes ni miongoni mwa viungo bora zaidi duniani kwa sasa na uwezo wake wa kufunga na kuchangia mabao ni wa kiwango cha juu sana.

Ushindi kwa Chelsea katika gozi la leo dhidi ya Man-United ugani Stamford Bridge, utawapaisha hadi nafasi ya nne jedwalini kwa alama 46, tatu nyuma ya Man-United ya kocha Ole Gunnar Solskjaer.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Polisi Kamukunji wachunguza kilichosababisha moto katika...

Aston Villa wapepeta Leeds United na kuweka hai matumaini...