Michezo

Nimeafikia lengo langu la kwanza Supa Ligi, asema Makumbi

May 22nd, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

VITA vya kuwania ubingwa wa ligi ya Supa vinazidi kuchacha huku Klabu ya Western Stima ikikwamilia kileleni baada ya mkondo wa kwanza wa ligi hiyo kukamilika.

Stima wanaongoza msimamo wa jedwali la ligi hiyo kwa alama 36 japo wamecheza mechi 18 ikilinganisha na klabu nyingine katika ligi hiyo. Timu nyingine aidha zimesakata mechi 16 au 17.

“Nilitaka kukamilisha mkondo wa kwanza wa mechi za ligi nikiwa kileleni na kwa mwanya mkubwa kati ya timu yangu na nambari mbili, Sasa tunalenga kuibuka na ubingwa katika mkondo wa pili,” akasema kocha wa Stima Richard Makumbi, Jumatatu.

Stima wana mwanya wa alama 4 kati yake na Klabu ya Ushuru ambao tayari wamesajili alama 32. Nairobi Stima wanafuata kwa alama 31 nao klabu za KCB na Kibera Black Stars zikiwa katika nafasi ya tatu na nne mtawalia kwa alama 30 ingawa wanabenki wana idadi ya juu ya mabao.

Western Stima wanaopania kurejea kwenye ligi kuu ya KPL,waliagana sare ya 1-1 na Talanta FC mechi iliyosakatwa ugani Camp Toyoyo siku ya Jumamosi.

Nairobi Stima nao waliwaduwaza KCB 2-1 katika mchuano uliogaragazwa Naivasha na kuendelea kushikilia nafasi ya pili.

Katika matokeo mengine, St Joseph Youth waliwanyeshea mabao 4-1 Kangemi All Stars ugani Afraha mjini Nakuru huku vijana wa Coast Stima wakizidisha masaibu ya Kenya Police kwa mabao 3-1.

Mechi ya pekee iliyosakatwa siku ya Jumapili iliwashuhudia Ushuru FC wakiwapepeta Bidco United 1-0 katika uwanja wa manispaa ya Thika.

Mkondo wa kwanza unapokamilika timu za Green Commandos, GFE105 na Nakuru All Stars zipo kwenye eneo hatari za kushushwa ngazi na itapidi wajikakamue katika mkondo wa pili kuepuka shoka la kutemwa hadi ligi ya chini.