Siasa

Nimechoka! Rais apuuza dai ana njama kurudi mamlakani na Raila 2022

October 16th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta amepuuzilia mbali wanasiasa wanaopinga shughuli za jopo la maridhiano alilounda na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, na kusema yeye binafsi hana haja kuundiwa nafasi ya kuendelea kuwa uongozini baada ya 2022 kama inavyoshukiwa na wakosoaji wa jopo hilo.

Akizungumza wakati wa kuzindua ujenzi wa barabara kuu ya moja kwa moja kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), hadi eneo la Westlands, Nairobi, Rais alisema wanaopinga jopo hilo lililo maarufu kama BBI ni wapotovu.

“Wanasema ati BBI ni Uhuru anataka kazi. Mimi sitaki kazi; nimechoka! Lengo la BBI ni kuhakikisha hakuna Mkenya atamwaga damu tena katika nchi yetu kwa sababu ya siasa,” akasema.

Jopo hilo hukashifiwa na baadhi ya viongozi wa Jubilee hasa wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto.

Viongozi hao wa kikundi cha ‘Tangatanga’ hudai waasisi wa BBI wanalenga kumzuia Dkt Ruto kuingia mamlakani ifikapo 2022, huku kukiwa na madai kwamba analenga kushirikiana na Rais Kenyatta ambaye ataundiwa nafasi maalum ya uongozi.

Hii ni kutokana na kwamba, kuna matarajio makubwa ripoti ya jopo hilo itakayowasilishwa kwa Rais wakati wowote mwezi huu itajumuisha hitaji la kuwepo nafasi za Waziri Mkuu mwenye mamlaka makuu ya uongozi pamoja na manaibu wake.

Lakini Rais Kenyatta alitaka wananchi wasipotoshwe na dhana hizo, akaonekana kutaka kila mmoja aunge mkono ripoti ya BBI inayosubiriwa kwa hamu.

“Hiyo safari najua mimi pamoja na ndugu yangu Raila tutaikamilisha pamoja na viongozi wengine wote wa Jamhuri hii ya Kenya. Kwa hivyo msidanganywe, mpende nchi yenu, mjipende nyinyi wenyewe, mjiheshimu na sina shaka tutatoboa hii safari,” akasema.

Kikatiba, Rais anatarajiwa kustaafu 2022 baada ya kuongoza nchi kwa awamu mbili tangu mwaka wa 2013.

Utawala wake umekumbwa na panda shuka, akikosolewa sana kuhusu madeni yaliyopita Sh6 trilioni, ufisadi, ahadi tele zisizotekelezwa, na mashambulio ya ugaidi yaliyokithiri wakati wa awamu yake ya kwanza ya uongozi.

Kisiasa, viongozi kadhaa wa ngome yake Mlima Kenya wameungana kumkaidi huku wale wa Rift Valley waliompigia debe uchaguzini wakimtenga na kusema anamsaliti Dkt Ruto.

Imesemekana ripoti ya BBI huenda ikawasilishwa kwa Rais kabla Sikukuu ya Mashujaa itakayofanyika mjini Mombasa Oktoba 20, ingawa jopo lilipewa muda hadi Oktoba 24 kukamilisha kazi yake.

Bw Odinga hutaka mfumo wa utawala ubadilishwe ili kuwe na nafasi ya Waziri Mkuu na manaibu wake, suala ambalo litahitaji kura ya maamuzi inayopingwa vikali na Dkt Ruto na wandani wake.