Habari Mseto

'Nimechoma maiti 8,000 Kariokor. Ni ajira ninayoienzi mno'

July 3rd, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

Bw Robert Mwania, mwanamume ambaye aliiteketeza maiti ya aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom katika makaburi ya kuchoma maiti ya Kariokor, Nairobi ameteketeza maiti takriban 8,000 hadi sasa.

Bw Mwania, ambaye ana zaidi ya miaka 60 amefanya kazi hiyo tangu 1997 na anasema kuwa ndiyo kazi aliyokuwa akiitamani tangu utotoni.

Kila siku, kazi yake ni kuandaa mili na kuichoma, akiona mtu akibadilika kuwa moshi na jivu, na sasa amezoea.

“Naipenda kazi yangu sana. Ndiyo inanipa riziki ya kila siku,” akasema Bw Mwania.

Anasema huwa anachoma kati ya mili 25 na 40 kila mwezi, kwa zaidi ya miaka 20 ambayo amefanya kazi hiyo.

Katika kazi yake hiyo, ameteketeza maiti za watu mashuhuri kama aliyekuwa waziri wa mazingira Prof Wangari Mathai, kando na Collymore, ambaye alimhudumia Jumanne.

“Nilihisi kuheshimika sana nilipomhudumia Prof Mathai,” akasema Bw Mwania.

Mahali pake pa kazi, anatumia kuni ama stima kuichoma mili. Mbeleni hata hivyo, kazi hiyo ilifanywa kwa kuchomwa na diseli.

Kuchoma maiti kwa kutumia kuni huchukua kama saa tatu, huku umeme ukitumia saa moja. Mili mitatu inaweza ikachomwa mara moja kwa wakati wowote ule katika sehemu ya kuni.

Bw Mwania anasema kuwa idadi ya watu weusi ambao wanaamua kuteketezwa wanapokufa imezidi kuongezeka siku za majuzi, hasa miaka mitatu iliyopita.

“Hii ni kwa kuwa wengi wao wanaona ni gharama kusafirisha maiti kwa safari ndefu hadi nyumbani,” akaeleza Bw Mwania.

Ili kuteketeza maiti ya mtu ambaye si wa dini ya Kihindi, familia hulipa Sh40,000, nao wale wa dini hiyo hulipa kati ya Sh18,000 na Sh24,000 kulingana na ikiwa watatumia stima ama kuni. Watoto wa chini ya miaka 10 hawawezi kuchomwa.