HabariSiasa

Nimechoshwa na huyu Ruto, Uhuru awaka

December 5th, 2019 1 min read

Na MWANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano alichemka dhidi ya naibu wake William Ruto akisema amechoka kwa siasa zake.

Akizungumza alipofungua zahanati katika eneo la Mang’u, Kaunti ya Kiambu, Rais Kenyatta alisema amechoka na siasa za kila mara za kundi la Tanga Tanga ambalo linaunga mkono Dkt Ruto kuwa rais 2022.

“Kabla ya ripoti ya BBI walikuwa wakipiga siasa kote. Sasa tumetoa ripoti wameanza siasa zingine. Tumefika pahali na tunasema tumechoka. Hawa ni watu ambao hawajui wanachofanya. Itakuwa hivi ama vile. Wakome kutupigia kelele kila mara,” akasema.

“Huwa wanaona nimenyamaza wanadhani mimi ni mjinga. Hakuna kitu ambacho sijui,” akaongeza.

Uhusiano kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto umeendelea kuzorota tangu handisheki mwaka jana.

Katika siku za majuzi Rais amekuwa akieleza wazi hisia kali dhidi ya naibu wake na wafuasi wake na kuwaeleza wasahau kuchaguliwa kwenye uchaguzi wa 2022.

“Ni Mungu na wananchi wanaojua atakayeongoza,” akasema.