Michezo

Nimefanyia wanasoka wa Harambee Stars mambo mengi makubwa bila ya kujigamba – Wanyama

May 21st, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BAADA ya Victor Wanyama kulaumiwa kwa uongozi wake kambini mwa Harambee Stars na kucheza kwa kujituma na kujitolea zaidi kila anapovalia jezi za timu ya taifa, kiungo huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur ameutetea ukapteni wake katika timu ya taifa ya Kenya.

Wanyama amekuwa akilaumiwa kwa kuafikiana na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kuhusu mambo muhimu yanayohusu kikosi kizima cha Stars, bila kushauriana na wanasoka wenzake.

Kwa mujibu wa beki Aboud Omar, Wanyama alifanya maamuzi kwa niaba ya Stars kuhusu marupurupu ambayo wachezaji wangepokezwa wakati wa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2019 nchini Misri bila ya kutaka kujua maoni na misimamo yao.

Aidha, nyota huyo wa zamani wa Celtic na Southampton amekuwa akishtumiwa kwa kukosa kupigania haki na maslahi ya wachezaji wenzake katika kikosi cha Stars huku akitakiwa sasa kuiga mfano wa kigogo Musa Otieno aliyewahi kuvalia utepe wa unahodha wa Stars kwa muda mrefu pindi baada ya kuingia katika timu ya taifa mnamo 1993.

Katika mahojiano yake na Madgoat TV, Wanyama alisema amejitolea kupigania bonasi za wanasoka wa Stars na alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba beki Brian Mandela anafanyiwa upasuaji nchini Ufaransa.

Mandela alipata jeraha baya la goti nchini Ufaransa ambako Stars walipiga kambi kabla ya fainali za AFCON mwaka 2019 chini ya aliyekuwa mkufunzi wao, Sebastien Migne.

Kwa mujibu wa Wanyama, ilihitaji juhudi zake binafsi kushawishi FKF kugharimia matibabu ya difenda huyo na kubatilisha mpango wa kumrejesha humu nchini pindi baada ya kujeruhiwa.

“Nisingekubali mmoja wetu akandamizwe kambini. Nilimpigania asafiri nasi hadi Misri hata baada ya kupata nafuu. Iwapo FKF ingekataa pendekezo langu, nilikuwa radhi kugharimia usafiri wa Mandela, malaji na malazi yake kwa kipindi kizima ambacho tungekuwa Misri kwa kipute cha AFCON,” akasema.

Wanyama ambaye kwa sasa anachezea Montreal Impact ya Canada, amesema kuwa alipigania pia beki Philemon Otieno wa Stars atibiwe na FKF japo juhudi zake zikaambulia patupu.

Otieno alipata jeraha la mguu mwaka 2019 Stars walipovaana na Tanzania kwenye mechi ya marudio ya kufuzu kwa fainali za CHAN ugani MISC Kasarani. Licha ya kuumia akiwajibikia timu ya taifa, Otieno alitegemea misaada ya wahisani na wasamaria wema ili kufanyiwa upasuaji.

Wanyama ameshikilia kwamba wakosoaji wake hawana ufahamu kuhusu ukubwa wa mchango wake katika makuzi ya soka ya humu nchini, kupigania maslahi ya wenzake na hata kuwatafutia baadhi ya chipukizi dili za kutamanisha katika mataifa ya kigeni.

“Nimekuwa nikisukumana sana na FKF na uhusiano wangu na baadhi ya vinara wa shirikisho hilo umevurugika kwa sasa kutokana na msimamo wangu. Si lazima kila kizuri ninachokifanya kifahamike kwa umma. Sipendi kujigamba,” akasema.