Habari Mseto

Nimegundua mume wangu ni mbichi mno chumbani, nitafanyaje?

January 8th, 2024 1 min read

Hujambo shangazi? Nimeolewa kwa miezi kadhaa. Hapo kabla ya ndoa tulikubaliana kwamba hatutaonja asali hadi tutakapooana. Sasa nimegundua ni mbichi sana katika masuala ya chumbani. Nifanye nini?

Sielewi unatarajia mume wako atoe wapi ujuzi wa mambo hayo ilhali ulimwambia msubiri hadi ndoa. Kama una ujuzi, usione aibu kumfunza jinsi ya kukupa raha. Kama huna, shirikiana naye mjifunze.

Nashindwa kuchagua mmoja, nitaoa wawili

Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 30. Nimeshindwa kuchagua mmoja wa wanawake wawili ambao wamenasa moyo wangu. Sasa nafikiria kuwachukua wote kuwa wapenzi wangu. Hofu yangu ni kuwa watajuana. Nifanye nini?

Haiwezekani kupenda wawili kwa wakati mmoja. Mimi kamwe siungi mkono ulaghai wa kimapenzi na siwezi kukusaidia kuwachezea wanawake hao. Hata ukifaulu, hatimaye watagundua mchezo wako.

Mpenzi mrembo mno ila natamani wengine nje!

Mpenzi wangu ni mrembo sana, wanaume wengi wakimuona humtamani. Ajabu kuwa nikiona wanawake wengine bado nawatamani. Ni kwa nini?

Aliyesema binadamu hatosheki hakukosea. Hata hivyo, amepewa uwezo wa kujizuia kuongozwa na tamaa. Unaungama kuwa umebahatika kupata mpenzi anayekufaa. Tulia kwake na umpe moyo wako wote.

Ameniacha kunishuku na jirani yetu, nipe ushauri

Nilikuwa nimeolewa lakini mume wangu akaniacha kwa kushuku nina uhusiano na jirani yetu. Ukweli ni kuwa jirani amekuwa akinitaka lakini nimemkataa. Nifanyeje?

Ni bahati mbaya kwamba mume wako alikuacha kwa kukushuku tu. Itabidi ukubali uamuzi wake. Kama aliyesababisha yote hayo yuko tayari kukuoa na unampenda, mkubali uendelee na maisha yako la sivyo utafute mwingine.