HabariSiasa

Nimekuwa nikishauriana na Rais kwa njia ya video kuzuia maambukizi – Ruto

April 10th, 2020 2 min read

NA CHARLES WASONGA

HATIMAYE Naibu Rais William amejitokeza na kuelezea sababu ya kutoonekana pamoja na Rais Uhuru Kenyatta kila mara anapohutubia taifa kuhusu janga la corona.

Akiongea na wanahabari katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Alhamisi Dkt Ruto alipuuzilia mbali madai kuwa ametengwa katika suala hilo akisema kuwa huwa anafanya mashauriano na Rais Uhuru Kenyatta kila mara kuhusu janga hilo.

“Mimi na Rais tumekuwa tukizingumza kila mara kuhusu mikakati ya kuisadia taifa hili kukabiliana na janga hili. Tumekuwa tukifanya mashauriano hayo kwa njia ya video ili kutii kanuni ya kutokaribiana,” akasema.

“Katika hali kama hii rais na naibu wake hawawezi kusafiri kwa chombo kimoja. Lakini huwa tunashauriana kila siku pamoja na mawaziri wengine ambao wamekuwa wakisimamisha shughuli za kudhibiti janga hili… na hiyo ndio msimamo wa utawala wa Jubilee,” Dkt Ruto akasisitiza.

Naibu Rais alisema maafisa wakuu serikali wamekumbatia mbinu ya kufanya mikutano kwa njia ya video (video conferencing) ili kuhakikisha kuwa maafisa waafiki hitaji la kutokaribiana.

Dkt Ruto hajaonekana katika vikao na wanahabari ambako Rais Kenyatta amekuwa akitumia kuwatangazia wananchi hatua ambazo serikali imechukua dhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.

Hatua hizo ni kama vile amri ya kutotoka nje kati ya saa moja usiku na saa kumi na moja alfajiri kote nchini na marufuku ya watu kutoingia wala kutotoka kaunti za Nairobi, Mombasa, Kwale na Kilifi.

Kutoonekana hadharani kwa Dkt Ruto kumechochea hisia mseto miongoni mwa Wakenya katika mitandao ya kijamii. Baadhi yao wamedai ametengwa huku wengine wakishikilia kuwa ametelekeza majukumu yake wakati ambapo taifa linakabiliwa na changamoto kubwa kiasi hiki.

“Hatimaye William Ruto amejitokeza leo kutuhubia taifa. Sijawahi kumwona Naibu Amiri Jeshi ambaye hujificha wakati wa changamoto la kitaifa. Sharti atoe sababu mwafaka zilizochangia kupotea kwake, kujificha, au kutelekeza majukumu yake ilhali anaendelea kupokea mshahara,” Abraham Mutahi akasema kupitia mtandao wa Twitter.

“Jameni, sijali kama marufuku inayoendelea kutekelezwa. Lakini nauliza, Je, Naibu Rais yuko wapi?” Mkenya aliyejitambulisha kama Mpile aliuliza kabla ya Dkt Ruto kuwahutubia wanahabari.

Wakati wa hotuba yake Naibu Rais alikariri yale ambayo Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na Rais Kenyatta wamekuwa wakisema katika hotuba zao kwa wananchini.

“Hili ni janga hatari zaidi kwa maisha yetu na uchumi wetu. Kwa hivyo, nawahimiza Wakenya wote kuzingatia masharti ambayo yametangazwa na serikali ili kuzuia kusambaa kwa virusi hivi,” Dkt Ruto akasema.