Makala

SHANGAZI: Nimeoa, yeye pia ameolewa, anataka tuwe wapenzi

February 19th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

Hujambo shangazi? Nilifungua biashara hivi majuzi na nimeajiri wafanyakazi kadhaa, wanaume kwa wanawake. Nilishangaa mfanyakazi mmoja wa kike alipokuja ofisini kwangu na kuniambia wazi kuwa ananipenda ingawa anajua nina familia naye pia ana mume. Ni mrembo sana na hatua yake hiyo imeamsha hisia zangu kwake ingawa sikuwa na nia hiyo nilipomuajiri. Nishauri.

Kupitia SMS

Mimi sijawahi na sitawahi kuunga mkono uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa. Wewe ni mume wa mtu na huyo unayedai anakutaka vile vile ni mke wa mwenyewe. Ni muhimu kila mmoja wenu kuheshimu ndoa yake na pia kudumisha heshima kati yenu kama mwajiri na mwajiriwa. Kama hamtaweza kujizuia basi ni heri umuachishe kazi.

Mama mkwe ataka kunipokonya mke

Hujambo shangazi? Nimeoa kwa miaka miwili na tumejaliwa mtoto mmoja. Lakini mama mkwe anatishia kuvunja ndoa yetu. Anadai kuwa mke wangu ndiye mtoto wake wa pekee na ameamua kuwa hawezi kuishi peke yake. Sasa anataka kumtoa kwangu kisha anirudishie mahari niliyomlipa. Nifanyeje nini?

Kupitia SMS

Sielewi ni kwa nini mama mkwe wako amebadili nia miaka miwili baada ya kukuruhusu kumuoa binti yake kwani hata wakati huo alijua ndiye bintiye wa pekee. Madai yake hayo ni kisingizio tu, ninaamini kuna sababu nyingine na inawezekana mke wako pia yuko katika njama hiyo kwa sababu hawezi kulazimishwa kutoka katika ndoa. Iwapo hali ni hiyo, huna budi kusalimu amri.

Mpango wa kando adai mimba ni yangu

Kwako shangazi. Nina mke lakini nimekuwa na uhusiano na mwanamke fulani kwa muda mfupi tu. Sasa nimegundua ana mimba na anadai ni yangu ilhali nimeonja asali mara moja tu. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ninaamini kuwa hilo litakuwa funzo kwako kwamba mahusiano nje ya ndoa yanaweza kukutia mashakani. Ndiyo, mimba inaweza kupatikana mara ya kwanza ya tendo la ndoa. Kama una hakika si yako, mwambie mwanamke huyo asubiri mtoto azaliwe kisha wewe naye mpimwe DNA ukweli ujulikane.

Nilimfukuza baada ya kumfumania na jirani, ataka kurudi
Shangazi nimekuja kwako unipe ushauri. Nilikuwa na mke lakini tukaachana nilipomfumania na mwanamume jirani yetu. Tulikuwa tumepata mtoto mmoja na alirudi naye kwa wazazi wake. Sasa amekuwa akinipigia simu akitaka turudiane. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Inawezekana kwamba mke wako aliteleza tu kwani ni binadamu tu. Hali kwamba anakulilia akitaka mrudiane ni ishara kwamba anajuta kwa kitendo chake na kwamba bado anakupenda wewe kama mume wake na baba ya mtoto wake. Tathmini moyo wako uone kama unaweza kumsamehe na kumpa nafasi tena katika maisha yako.

Hatangazi msimamo kuhusu penzi letu

Shikamoo shangazi? Nina umri wa miaka 20 na kuna kijana ninayempenda sana na anajua kwa hakika kuwa nampenda. Nimekuwa nikimhakikishia penzi langu kwake lakini yeye hunyamaza tu, hajaniambia iwapo ananipenda au la. Najua ananipenda lakini sijaona ishara yoyote kutoka kwake ya kuthibitisha hilo. Nishauri.

Kupitia SMS

Inaonekana kuwa wewe ndiye unayempenda kijana huyo, labda yeye hana hisia zozote kwako. Sababu ni kuwa hajawahi kukwambia anakupenda hata siku ulipoungama penzi lako kwake. Chunga usije ukawa unafuata upepo tu huku ukiamini unapendwa ilhali yeye hana haja nawe.

Jembe huuma likikaa sana kama halijalima

Hujambo shangazi? Mimi ni mwanamume mwenye umri wa makamo na nina tatizo ambalo linanisumbua. Nimekuwa nikipatwa na maumivu makali katika sehemu zangu nyeti hasa ninapokaa muda mrefu bila burudani. Shida ni nini?

Kupitia SMS

Hilo ni tatizo linalohitaji kushughulikiwa kimatibabu na mimi ni mshauri tu wala si daktari. Nenda hospitalini ukaguliwe ili shida ijulikane na ikiwezekana utibiwe.