Shangazi Akujibu

Nimetupa ndoano, nikatuma hata rafikiye, lakini bado samaki hamezi chambo

May 20th, 2024 1 min read

Kuna mwanamke ninayempenda kwa moyo wangu wote lakini amenikataa. Juzi nilimtuma rafiki yake amwelezee ninavyompenda akamwambia niende kwake mwenyewe nimwambie. Nifanyeje?

Kama mwanamke huyo alikwambia hakutaki, sidhani amebadili msimamo wake huo baada ya kutumana kwake. Lakini tunaambiwa atafutaye hachoki. Kama amekualika nenda.

Mapenzi yameisha kwa mume wangu, niko tu!

Shangazi, nilikutana na mume wangu siku chache baada ya kuachana na mpenzi wangu. Tumezaa mtoto lakini hisia zangu kwake zimetoweka ingawa najua ananipenda. Sitaki kuishi na mtu nisiyempenda. Nifanye nini?

Ndoa isiyo na mapenzi ina changamoto nyingi. Ni muhimu mume wako ajue kuhusu unavyohisi. Haitakuwa rahisi kwake hasa kama anakupenda. Lakini hiyo ndiyo jinsi pekee ya kutatua tatizo lako.

Nahisi kuna jambo linatokota na hasemi

Hujambo Shangazi? Nimeanza kuona dalili zisizo nzuri kati yangu na mpenzi wangu. Wiki tatu sasa zimepita hajanipigia simu wala kunitumia ujumbe na hiyo si kawaida. Nina wasiwasi. Nipe ushauri.

Usiendelee kunyamazia hali hiyo. Mtafute mpenzi wako akwambie nia yake hasa. Kama ameamua kuvunja uhusiano wenu atakwambia ili upate nafasi ya kuendelea na maisha yako.

Kidosho ananitaka cha lazima!

Kuna mwanamke jirani katika mtaa ninamoishi ambaye amekuwa akinitaka lakini simtaki. Nilioa majuzi na nimegundua ameanza kumpa mke wangu udaku ili aniache. Nifanyeje?

Ninaamini ndoa yenu imetokana na mapenzi ya dhati wala si mambo mengine. Kama ndivyo, mke wako hawezi kukuacha kutokana na udaku anaopewa na jirani yenu. Ondoa hofu.