Habari

Nina mipango ya kuwaokoa, Ruto aambia wakulima

Na MWANGI MUIRURI August 10th, 2024 2 min read

RAIS William Ruto amesisitiza kuwa ana mipango ya kuimarisha sekta ya kilimo akisema atahakikisha wakulima wadogo wanapata faida kwa juhudi zao, kuwaondoa mabroka na hata kuwapa mikopo ya riba ya chini.

Rais alisema kuwa serikali yake imetenga Sh5.7 bilioni kwa wakulima wa kahawa kama njia ya kuwaokoa dhidi ya mashirika yanayotoa mikopo ya riba ya juu.

Kiongozi wa nchi alisema mpango wake ni wakulima wawe wanapata mikopo kwa riba ya asilimia tatu kutoka kwa Hazina ya Mzunguko ya Kahawa(CCARF).

Aliongeza kuwa mageuzi ya sekta ya kilimo ambayo utawala wake unaendesha pia utashuhudia wakulima wa chai wakipokea Sh210 bilioni kutoka Sh170 bilioni mwaka jana.

“Hatutafanya mchezo katika sekta hii ya kilimo. Nimemwagiza Naibu Rais Rigathi Gachagua kunyoosha sekta hiyo na kuwaondoa mabroka wanaohujumu ajenda yetu ya kufufua sekta ya kilimo,” Rais alisema.

Bw Gachagua alisema kazi ya kukabiliana na mabroka katika sekta ya kilimo ndiyo kazi ngumu zaidi ambayo rais amemkabidhi kama msaidizi wake mkuu.

Alisema sekta ya makadamia imefanyiwa marekebisho akisema bei kwa sasa ni Sh120 kwa kilo kutoka Sh20 ambazo mabroka walikuwa wametekeleza miezi mitano iliyopita.

Bw Gachagua alimshukuru rais kwa kuagiza kutengwa kwa Sh7 bilioni ili kulipa madeni ya kahawa nchini.

Bw Gachagua aliwataka wakulima nchini waungane ili wawe na sauti thabiti itakayowawezesha kuchochea mabadiliko ya sera yanayotarajiwa.

‘Umoja wenu ndio umuhimu wenu, kuzungumza kwa sauti moja ndilo jambo la msingi,” akaongeza Bw Gachagua.

Dkt Ruto pia alisema kuwa aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mithika Linturi alifutwa kazi kwa sababu alishindwa kuboresha sekta ya kilimo.

Hata hivyo, Rais alisikitika kwamba ajenda yake ya maendeleo itadidimia kwa sababu ya kukosekana kwa utulivu wa kisiasa pamoja na matatizo ya kisheria ambayo yalimfanya aondoe Mswada wa Fedha wa 2024.

‘Kulikuwa na matatizo ambayo yalifanya bajeti yangu ya utoaji wa huduma kuporomoka. Miradi yangu mingi ya maendeleo imeathiriwa baada ya bajeti kupunguzwa lakini nitajitahidi kutumia kile nilichonacho,’ Rais Ruto alisema akiwa Kiria-ini.

Kando na hayo, Rais alisema Murang’a itapata Sh1 bilioni za kuunganisha umeme na Sh1.1bilioni za barabara. Dkt Ruto alimtambulisha Waziri mpya wa Nishati Bw Opiyo Wandayi akisema ataleta mabadiliko katika sekta hiyo kwa kuunganisha umeme.

Pia alitangaza kutenga Sh1.2 bilioni kujenga masoko 20 kama njia ya kuheshimu biashara ya mama mboga.