Habari

Nina pesa nyingi kama njugu – Waititu

June 7th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

GAVANA wa Kiambu, Ferdinand Waititu, amewaonya mahasidi wake wa kisiasa kuwa lau wangeelewa ukwasi halisi alio nao, hawangepoteza wakati wao wakimwandama bali wangezirai tu kwa mshtuko.

“Mimi nilijipanga kitambo kihela na wewe ukiwa bado unahangaika ukisaka utajiri, jua mimi nilikutangulia kufika kileleni buana; acha mchezo,” akasema Jumatano katika mahojiano ya moja kwa moja na Taifa Leo.

Waititu alitaja aliyekuwa Gavana wa Kiambu, William Kabogo, Seneta Kimani Wamatangi, naibu gavana James Nyoro na Kasisi David Ngari kama walengwa wa ujumbe wake, akiwataka wajiandae kwa kivumbi ikiwa wameamua kuwania ugavana mwaka 2022.

Aliwatahadharisha kiasi cha kusema historia imebainisha Wakenya huwa na mazoea ya kuchagua wanasiasa wanaopigwa vita zaidi, akitaja mwenzake wa Embu Nyaga Wamborah, wa Makueni Kivutha Kibwana na yule wa Murang’a Mwangi Wa Iria kama ushahidi wake.

“Hawa kwa wakati mmoja waling’atuliwa na mabunge yao lakini hadi sasa ni magavana. Kura huwa na wapigakura waliosajiliwa katika eneo unalowania,” akasema.

Bw Waititu alisema kuwa ikiwa anaandamwa kwa msingi wa kisiasa, hasa kwa kujihusisha na siasa za kuegemea mrengo wa Naibu Rais Dkt William Ruto kama mfaafu kuwa Rais mwaka 2022, asidhaniwe kuwa mwepesi nyanjani “na ambapo nimekiri wazi kuwa cha kuniogofya na kunitia kiwewe ni hasira ya Mungu na uji moto.”

“Mimi ni Baba yao,” akasema.

Utajiri

Waititu alisema kuwa pesa zake alianza kuziunda miaka 30 iliyopita wakati alijinunulia malori mawili ya kuchuuza malighafi ya ujenzi katika eneo la Mashariki mwa Nairobi.

“Malori hayo yalizidi na yakawa 25. Nikanunua matingatinga ya kuchimba ploti kwa wawekezaji eneo hilo. Nilikuwa diwani, Naibu wa Meya, waziri msaidizi, mbunge na sasa Gavana. Kwa miaka 30 mimi nimekuwa nikijikusanyia mali kwa dhati ili nihepe umaskini uliokuwa unanibishia mlango miaka ya sabini (1970s),” akasema.

Waititu alisema kuwa hata baadhi ya wanasiasa wakifanikiwa kumuaibisha awekwe kwa seli za polisi, “mimi ni mtu wa kawaida kwa masaibu ya aina hiyo na nitalala kwa seli hizo na ning’orote nakuambia.”

Alisema kuwa mali anayodaiwa kujipa kwa muda mfupi ni mali yake halisi na halali na hana suala la kuomba msamaha.

“Mimi leo hii ni muuzaji, mwekezaji na dalali wa kila aina ya mali jijini. Nina zaidi ya hekari 200 za vipande vya ardhi Nairobi ambazo huwa nauza kama ploti. Kusema nimenunua nyumba ya thamani ya Sh680 milioni sio suala la kubabaisha. Kuna vile nimejipanga na niko na madeni tele ambayo nazidi kulipia. Wewe baki hapo ukishangaa na ukinisemasema badala ya kutumia wakati wako kujijenga,” akasema.

Aliwataka wote wanaompiga vita vya kisiasa wajiepushane na “kuwajumuisha baadhi ya watoto wangu na pia mke wangu” na badala yake wamwendee mwenyewe.

“Wanaume kamili ni kuonana, sio kuviziana kama sokwe mwituni,” akasema.

Aliwataka wote wanaochangia mjadala wa masaibu yake ndani ya vita dhidi ya ufisadi waelewe kuwa katika “afisi za tume ya kupambana na ufisadi (EACC) na ile ya Uchunguzi wa jinai (DCI) kumefunguliwa faili za kupokea ushahidi kuhusu ufisadi huo wangu unaoujua.”

Aliwataka wawe wangwana na wafike mbele ya maafisa katika afisi hizo na wawasilishe ushahidi huo badala ya kuuropoka katika hafla za “mazishi, uchumba na ulipaji mahari.”