Habari MsetoSiasa

Nina ushahidi wa kuthibitisha Joho ni mlanguzi wa mihadarati – Gavana Sang

February 5th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MALUMBANO baina ya Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho na mwenzake wa Nandi Stephen Sang’ kuhusu mihadarati yaliendelea kushamiri Jumanne pale Bw Sang’ alipoapa kwamba hatamwomba msamaha Joho kwa kumhusisha na ulanguzi wa dawa hizo za kulevya.

Bw Sang’ aliahidi kuwasilisha ushahidi katika Idara ya Upelelezi wa Jina (DCI), baada ya wiki mmoja, kuonyesha kuwa Bw Joho amekuwa akishiriki biashara hiyo haramu kwa muda mrefu.

“Siwezi kumwomba Joho msamaha kwa kusema ukweli kwamba yeye ni mlanguzi wa mihadarati. Na nina ushahidi wa kuthibitisha madai yangu na sitayawasilisha kwake vile alivyopendekeza bali nitayawasilisha kwa DCI na Interpol (Polisi wa Kimataifa) baada ya wiki mmoja hivi,” akasema kwenye kikao na wanahabari katika mkahawa wa Serena, Nairobi.

Bw Sang’ alimtaka mwenzake kuwaomba msamaha vijana wa taifa hili, haswa wanaotoka Mombasa, ambao alidai maisha yao yameharibisha na dawa hizo haramu huku akimtaka kukoma kuingiza jina la Naibu Rais William Ruto katika suala hilo.

“Kama kiongozi kijana, sitakoma kutetea masilahi ya vijana wenzangu ambao wameharibiwa na biashara hii, hasa huko Mombasa ambako Joho mwenye anatoka. Kwa hivyo, nitaendelea kupambana na jinamizi hilo mpaka mwisho,” akasema huku akidai kuwa Bw Joho ni mshirika wa ndugu wawili ambao wamezuiwa nchini Amerika kwa kupatikana na hatia ya kushiriki ulanguzi wa dawa za kulevya.

“Kwa hivyo, Joho asiwapotoshe Wakenya kwa kuingiza jina la Naibu wa Rais katika suala hili kwa sababu nililizungumzia kwa niaba yangu kama kiongozi aliyechaguliwa na wananchi. Sikutafuta ushauri kutoka kwa mtu yeyote,” Bw Sang’ akasema.

Mnamo Jumatatu Bw Joho alidai kuwa gavana Sang’ na wabunge wengine wa Jubilee walitumwa na Dkt Ruto kumharibia jina kwa kumhusisha na biashara ya mihadarari.

“Mimi siwezi kujibizana na watu ambao siwajui. Najua wametumwa na mkuu wao ambaye ni William Ruto. Anafaa kuwa jasiri na kukabiliana name,” akasema alipoandamana na mgombeaji wa ODM katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Embakasi Kusini Irshad Sumra alipokuwa akiwasilisha stakabadhi zake kwa IEBC.

Lakini Bw Sang’ amedai Bw Joho tayari hana heshima baada ya kile alichodai ni ufichuzi wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) kwamba alighushi cheti cha masomo ili aweze kuidhinishwa kuwania kiti cha ugavana wa Mombasa.

“Bw Joho hana heshima ya kuharibiwa kwa sababu tayari KNEC ilithibitisha kuwa yeye ni mlaghai,” akasema. Hata hivyo, suala hilo liliwasilishwa mhakamani mnamo 2015 na Gavana Joho akaondolewa lawama.

Majuma mawili yaliyopita Bw Sang’ alisema Bw Joho hafai kumshambulia Dkt Ruto kila mara katika mikutano yake ya hadhara ilhali “inajulikana wazi kuwa yeye, Joho, ni mlanguzi wa dawa za kulevya” ambaye amezuiliwa kuingia Amerika kwa kuhusishwa na uovu huo.

Alitoa madai hayo alipowahutubia waumini katika kanisa la St Francis of Assisi Cheptarit, katika kaunti ya Nandi, akiandamana na wabunge Oscar Sudi (Kapseret) na Didmus Barasa (Kimilili).